Kamati ya Bunge yaiagiza TPA

Muktasari:

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inasimamia usalama wa mizigo ya wateja inayoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inasimamia usalama wa mizigo ya wateja inayoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Pia, imewataka watumishi wa TPA kutojifungia ndani bali watoke kwenda kujifunza katika bandari za nchi zinginezo namna wanavyofanya kazi ili waingie katika mfumo wa ushindani.

Maagizo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso, baada ya kufanya ziara ya kiutendaji katika bandari hiyo.

“Mtenge kitengo cha masoko ili kwenda katika nchi zinginezo kutafuta wateja. Bandari ya Dar es Salaam imefanyiwa maboresho makubwa, meli kubwa zinaweka nanga, zinapakua mizigo kwa muda mfupi,” amesema Kakoso.

Mwenyekiti huyo pia ameshauri asilimia 40 ya mapato yanayokusanywa katika Bandari ya Dar es Salaam yanapaswa kuachwa TPA ili yatumike katika shughuli za maendeleo bandarini hapo, kuliko utaratibu wa sasa ambao makusanyo yote yanapelekwa serikalini.

Akizungumzia hali ya utendaji bandarini Naibu Mkurugenzi Mkuu TPA, Mhandisi Karim Mataka, “Kwa sasa hakuna urasimu kwa sababu tumekuwa tukishirikiana na mamlaka zinginezo kufanya kazi kama vile Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Amesema kwa sasa wameondoa vizuizi vilivyokuwa sumbufu, TANROADS wameondoa kero katika mizani iliyokuwa ikilalamikiwa na wafanyabiashara kwa kubakiza mizani miwili pekee ya upimaji.

Kuhusu udanganyifu wa bidhaa kwa wateja pindi wanapoingiza mizigo bandarini, Mhandisi Mataka alisema; “Tumedhibiti hali hiyo. Kwa sasa tuna mashine za ukaguzi nane eneo la bandarini, pia tuna mbwa wenye uwezo wa kukagua mizigo. Pia tumefanikiwa kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya”.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amesema serikali imefanya maboresho makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa ukusanyaji mapato.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikipitisha mizigo mingi kwenda nchi za jirani ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) asilimia 37, Malawi asilimia saba, Burundi asilimia tano, Rwanda asilimia saba na Uganda asilimia mbili.

Mwakibete alisema; “Mikakati ya Serikali ni kuhakikisha soko lote la nchi zisizokuwa na bahari linakamatwa na TPA, mizigo yao yote inapitia Tanzania”.