Kashfa ya utesaji watoto magerezani

Muktasari:

  • Timu ya wachunguzi ya tume hiyo ilitembelea magereza na vituo vya polisi 102 katika mikoa 12 nchini na walikutana na watoto 570, kati yao wakiwa ni watoto wachanga 47 waliokuwa na  mama zao gerezani.

Dar es Salaam. Ripoti mpya imebaini kuwapo kwa unyanyasaji mkubwa wa watoto wanaoshikiliwa kwenye magereza na mahabusu mbalimbali nchini.

Ripoti hiyo yenye kurasa 94 iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyochunguza hali za watoto magerezani na kwenye vituo vya polisi kwa mwaka 2012 na 2013, imebainisha kuwa walikamatwa kwa makosa mbalimbali yakiwamo wizi wa kutumia silaha, dawa za kulevya, mauaji, ubakaji na uzururaji.

Timu ya wachunguzi ya tume hiyo ilitembelea magereza na vituo vya polisi 102 katika mikoa 12 nchini na walikutana na watoto 570, kati yao wakiwa ni watoto wachanga 47 waliokuwa na  mama zao gerezani.

Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa watoto 452 walikutwa kwenye magereza ya watu wazima kinyume cha sheria, kati yao wavulana 414 na wasichana 38 na kubainisha kuwapo kwa watoto 1,250 wanaozuiliwa kwenye magereza ya watu wazima, nchi nzima.

“Wavulana 314 na wasichana 37 walikuwa bado wanasubiri hukumu, lakini watoto 101 (wavulana 100 na msichana mmoja), walikuwa wameshahukumiwa,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya watoto 65 walikutwa wakishikiliwa kwenye mahabusu nne zilizotembelewa, wakiwamo wavulana 59 na wasichana sita.

“Katika Shule ya Maadilisho ya Mbeya, walikutwa watoto 36 wote wakiwa ni wavulana, wakati uwezo wa shule ni kuhifadhi watoto 340 waliohukumiwa,” inaeleza ripoti hiyo.

Inazidi kueleza kuwa hata watoto wadogo ambao bado wananyonya, wamekuwa wakijikuta kwenye mateso kutokana na wazazi wao kushikiliwa kwenye vituo vya polisi kwa zaidi ya saa 24.

“Watoto 47 walikutwa vizuizini wakiwa wameambatana na mama zao. Watoto 17 walikuwa na umri wa chini ya miezi 12,” inaweka wazi ripoti hiyo.

Iliongeza kuwa watoto waliohojiwa na timu ya utafiti waliwatupia polisi lawama kwamba wamekuwa wakiwakamata bila kuwaambia makosa yao, huku wengi wakilalamika kwa kushushiwa kipigo na kuteswa na polisi hao.

Ripoti inasema kuwa ingawa ni matakwa ya kisheria kwamba kila mtu anayekamatwa ajulishwe kosa lake, lakini asilimia 79.6 ya watoto waliohojiwa kwenye vituo vya polisi walisema hawakuambiwa makosa yao.

Jumla ya watoto 182 kati ya 227 waliohojiwa kwenye magereza ya watu wazima, sawa na asilimia 80, walisema wamekuwa wakiishi na wafungwa watu wazima na kwamba wakati wa ukaguzi, walikutwa wafungwa 16,713 katika katika gereza lililostahili kuwa na wafungwa 11,142.

“Hali mbaya zaidi, wakati watoto wanapochanganywa na watu wazima mchana na usiku. Katika baadhi ya magereza watoto wenye umri chini ya miaka 18 hutenganishwa na watu wazima wakati wa usiku,” inasema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Helen Kijo-Bisimba, alisema njia pekee itakayowaweka salama watoto wanaozuiliwa magerezani ni kuwajengea majengo maalumu, ambako wataishi kwa amani.

Kijo-Bisimba alisema kwa kuwa mtoto anayenyonya, anahitaji kuwa na mama yake wakati wote hivyo, Serikali inatakiwa kuwapa wanawake wanaonyonyesha adhabu itakayowaepusha watoto wao na madhara ya kuishi gerezani.

Alibainisha kuwa, ripoti hiyo itasaidia kufichua hali ilivyo ndani ya magereza kwa kuwa wanaharakati wengi hushindwa kwenda kushuhudia mambo yanayoendelea kutokana na sheria kuwazuia kufanya hivyo.

“Huwa wanasema hakuna watoto wanaochanganywa na watu wazima, sasa naona ripoti hiyo itasaidia kuweka wazi,” alisema na kuongeza kuwa Serikali iongeze bajeti ya ujenzi wa magereza.