Kaya saba zakosa makazi, Mto Kiwira ukiporomosha udongo

Monekano wa mmomonyoko wa udongo uliofukia mto Kiwira  Wilaya ya Rungwe  unaotiririsha  maji katika Ziwa Nyasa Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Jaffar Huniu amesema nyumba saba zimeharibika na nyingine 34 ziko hatari baada ya barabara ya inayounganisha Vijiji Kapugi na Lyenje kuharibika kufuatia maji ya Mto Kiwira kumong’onyoa udongo.

Mbeya. Maisha ya wananchi wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya yako hatarini, baada ya maji ya Mto Kiwira kumong’onyoa udongo na kuharibu barabara inayounganisha vijiji Kapugi na Lyenje na nyumba saba, huku nyingine 34 zikiwa hatarini.

 Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Huniu amewataka wananchi wa kijiji cha Lwenje kuchukua tahadhari na maporomoko ya udongo.

Mto Kiwira hutiririsha maji yake katika Ziwa Nyasa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Leo Jumamosi Aprili 20, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Haniu amesema kadhia hiyo imetokea jana Aprili 19, 2024 baada ya mvua kubwa kunyesha mfululizo katika maeneo mbalimbali wilayani huko.

"Hali hiyo imesababishwa na mvua kubwa kunyesha na kusababisha udongo kunyonya maji kwa wingi na kuwepo kwa mseleleko wa udongo ambao umesababisha Mto Kiwira kufunikwa na madhara kwa kaya saba ambazo hazina mahala pa kuishi.

"Baada ya kupata taarifa, nimefika eneo la tukio kujionea uhalisia na tayari ametoa maelekezo kwa Tarura (Wakala ya Barabara za mijini na vijiji) kufanya utafiti wa athari na kuharakisha kuanza matengenezo," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Huniu akitembelea eneo la Mto Kiwira lililokumbwa na mmonyoko wa udongo kufuatia kukatika mawasiliano ya barabara  kutokana  na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha

Huniu amesema kuwa eneo la bonde la Mto Kiwira ni maarufu kwa kilimo cha kahawa, migomba na mahindi, wakulima wamepewa tahadhari kuwa makini, ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokea kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Wakati huohuo, ametoa maelekezo kwa Tarura kuharakisha kufanya tathimini ya barabara ya Kapugi-Ilenje kwenda Kijiji cha Ikuti iliyokata mawasiliano Aprili 16 mwaka huu.

"Kwa niaba ya Serikali niombe wananchi kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya wataalamu, ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) uwepo wa mvua nyingi," amesema.

Akizungumzia kadhia hiyo, mkazi wa Kijjji cha Ikuti, Nelly Aloyce amesema kukatika kwa barabara hiyo kumewafanya washindwe kwenda kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo mnada wa mazao.

"Tunaomba Serikali sikivu iharakishe kurejesha mawasiliano tutakufa njaa na familia, kwani wananchi wengi tunategemea kilimo kuendesha maisha yetu," amesema.