Kesi ya Chavda ya miaka 21 iliyopita yaanza kusikilizwa

Mfanyabiashara na raia wa India Pravinchandra Chauda(73)( kulia) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa mashtaka mawili ambayo ni kutoa taarifa za uongo Kituo Kikuu cha Polisi ( Central) Dar es Salaam na kujipatia mali kinyume cha sheria. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Katika macho ya sheria jinai huwa haiozi kama mtuhumiwa anakuwa hai hata ipite miaka mingi kiasi gani lakini ipo siku akibainika atachukuliwa hatua za kisheria, na hili limetimia baada ya mfanyabiashara jijini Dar es Salaam , kupandishwa kizimbani akituhumiwa kujipatia kiwanja Kwa njia za udanganyifu, kosa alilolitenda miaka miaka 21 iliyopita  na kudanganya kupotolewa na hati za viwanja hivyo.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara mzee mwenye umri wa miaka 73, Pravinchandra Girdharlal Chavda amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kwa kesi ya jinai akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujisingizia kupotelewa hati ya umiliki kiwanja.

Chavda, Mtanzania mkazi wa mtaa wa Nyang'oro, Upanga Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani mahakamani hapo jana Jumatatu, Oktoba 23, 2023  jioni baada ya kukamatwa na kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central).

Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, amemsomea mashtaka mawili, moja la kujipatia mali kwa  njia za udanganyifu kinyume cha vifungu 301 na 302 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code - PC) na lingine kutoa taarifa za uwongo kinyume cha kifungu cha 122(a) cha PC.

Katika shtaka la kwanza, Wakili Mwanga amedai kuwa Januari 10, 2002, Chavda alijipatia kiwanja kitalu namba 1,814 kilichopo Msasani Peninsula jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha kwa msajili wa hati nyaraka za uongo.

Wakili Mwanga amedai kuwa mshtakiwa huyo aliwasilisha nyaraka za uhamisho akijifanya kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji pekee wa Kampuni ya Central Point Investment Limited, inayomilili kiwanja hicho, wakati akijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la pili wakili Mwanga amedai kuwa Oktoba 7, 2019, katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Chavda alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Jeshi la Polisi.

Amedai kuwa siku hiyo mshtakiwa huyo alitoa taarifa za uwongo kwa maofisa hao wa Polisi kuhusiana na kupotea kwa hati miliki 5 kwa nia ya kujipatia taarifa ya upotevu wa nyaraka hizo, akijua kuwa si kweli.

Hata hivyo mshtakiwa huyo anayewakilishwa na wakili Majura Magafu amekana mashtaka yote kuwa si ya kweli.

Wakili Mwanga ameieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na akaiomba Mahakama ipange tarehe ya usikilizwaji wa awali kwa ajili ya kumsonea mshtakiwa muhtasari wa kesi

Kuhusu suala la dhamana wakili Mwanga ameieleza mahakama kuwa Upande wa mashtaka hauna pingamizi kwa kuwa mashtaka yanayomkabili mshtakiwa huyo yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo ameiomba Mahakama izingatie matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kutoa masharti Ili kuhakikisha kwamba mshtakiwa anapatikana mahakamani kwa tarehe ambazo Mahakama itakuwa inapanga kuendelea  na kesi hiyo.

Hakimu Mfawidhi Aaron Mathias anayesikiliza kesi hiyo amesema kuwa dhamana ya mshtakiwa huyo Iko wazi masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Mshtakiwa huyo ametimiza sharti hilo na akaachiwa huru kwa dhamana.

Hakimu Mathias amepanga kesi hiyo kuendelea Novemba 23, mwaka huu kwa ajili usikilizwaji huo wa awali.