Kigamboni wataja kinachokwamisha maendeleo yao

Wakazi wa Kigamboni wakitoa kero zao za miundombinu  kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyetembelea eneo hilo.

Muktasari:

  • Waiomba Serikali kutatua changamoto ya miundombinu ya barabara

Dar es Salaam. Wananchi wa Kigamboni wamewasilisha changamoto tatu zinazokwamisha kasi ya shughuli zao za kiuchumi, ikiwamo ubovu wa miundombinu ya Barabara ya Kibada-Mwasonga hadi Kimbiji.

Zingine ni kukosekana mitaro ya maji na changamoto ya kivuko cha Kigamboni.

Wamewasilisha hayo jana Jumatatu Aprili 29, 2024 mbele ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyetembelea Kigamboni kukagua kazi ya urejeshaji wa mawasiliano ya miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua.

"Barabara hii ya kilomita 41 ya Kibada-Mwasonga- Kimbiji imekuwa na ahadi nyingi tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami kuepuka adha tunayopata," amesema Amin Sambo, mkazi wa Kibada.

Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amesema barabara hiyo inategemewa na watu kutoka kata nne na kuna viwanda vikubwa 10.

Amesema amepambana kwa muda mrefu kudai barabara hiyo ijengwe kiwango cha lami, lakini haijajengwa.

Waziri Bashungwa amesema baada ya mvua kuisha wanajipanga kurejesha miundombinu yote iliyoharibiwa kupitia kitengo cha dharura cha Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

"Hata barabara hii maeneo yenye mikwamo makandarasi watakuja kurudisha mawasiliano lakini habari iliyo njema Serikali imetoa kibali cha ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami,” amesema Waziri Bashungwa.

Amesema mkandarasi ameshapatikana wa kujenga kilomita 41 kwa kiwango cha lami na wameongeza kilomita 10 kufikia jumla ya 51.

Mkazi wa Magogoni, Gemino Assenga amesema kilio chao ni maji yaliyotanda na kusababisha barabara kutopitika.

"Tunashangaa waziri unatupa mwezi mmoja wa kuendelea kusubiri ni kitu kigumu kwetu tunakuomba utatue kero ya maji ya barabara kwa sasa halafu mengine tutavumilia," amesema

Amesema yeye ana mtoto anasoma Shule ya Msingi Tungi ana mwezi mzima sasa hajaenda shule kutokana na adha ya maji kujaa barabarani.

"Tunaomba dawa za kudhibiti maji tunayotumia ili tusipate magonjwa ya mlipuko kwa sasa hali ni mbaya," amesema.

Waziri Bashungwa amesema yote anayafanyia kazi na hata yanayohusu wizara nyingine atayafikisha sehemu husika.

Kuhusu mifereji ya maji Waziri Bashungwa amesema ataunda timu kwenda kufanya usanifu wa kina na watakuwa wanaripoti kwa Mkuu wa Mkoa.