Kinachoendelea ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akizungumza wakati akkijibu maswali ya wabunge leo Jumanne, Aprili 16 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali kupitia TPA imetenga Sh22 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi Bandari ya Bagamoyo.

 Dodoma. Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetenga Sh22 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema hayo bungeni leo Jumanne Aprili 16, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu.

Mbunge huyo amehoji mpango wa ujenzi wa bandari hiyo umefikia hatua gani ya utekelezaji.

Kihenzile amesema Serikali kupitia TPA imekamilisha kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha eneo la mradi lenye ukubwa wa hekta 887.

Amesema kwa sasa mradi upo hatua za mwisho za ukamilishaji wa uhuishaji wa taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliofanyika mwaka 2010.

Naibu waziri amesema kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/2024, ili kuanza hatua za ununuzi kwa mkandarasi atakayejenga bandari hiyo.

“Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia TPA imetenga Sh22 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo,” amesema.

Amesema ujenzi utafanyika kwa awamu kulingana na matarajio ya ukuaji wa shehena na ongezeko la meli.

Kihenzile amesema awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa magati matatu yenye jumla ya urefu wa mita 1,000 na kina cha zaidi ya mita 15.5.

Amesema ujenzi wa bandari hiyo ni wa kimkakati kwa kuwa itachochea shughuli za viwanda na biashara katika eneo la Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (SEZ).

Kwa nyakati tofauti kumekuwa na mjadala kuhusu utekelezaji wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

Hayati Rais John Magufuli, akiwa madarakani alieleza ujenzi wa bandari hiyo una masharti magumu ya uwekezaji, ndiyo sababu ya kusuasua kutekelezwa.

Miongoni mwa masharti hayo alisema ni baada ya ujenzi kukamilika, Tanzania haitaruhusiwa kujenga na kuendeleza bandari nyingine yoyote ya Pwani ya Bahari ya Hindi kuanzia Tanga mpaka Mtwara.

Aprili 8, 2021, aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai aliitaka Serikali kuangalia upya mradi wa bandari hiyo, iwapo jambo hilo jema waendelee nao.

Ndugai, ambaye ni mbunge wa Kongwa alitoa ushauri wakati wa mjadala wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano (2021/22 hadi 2025/26).

Juni 26, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara (TBNC) jijini Dar es Salaam, alitangaza kuanza kwa mazungumzo ya kufufua mradi huo pamoja na ule wa chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga.