Kinana alivyojibu hoja nne za Chadema, Lissu afafanua

Kinana akizungumza na wanaCCM jijini Dodoma.

Muktasari:

Kinana amesema kuwa kushinda hakutokani na katiba mpya, wala tume huru ya uvchaguzi bali kuchagua viongozi wanaokubalika na  sera nzuri.

Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa CCM -Bara, Abdulrahman Kinana amewajibu Chadema kuwa hoja zao za Katiba mpya, sheria za uchaguzi, Rais Mzanzibari na majimbo zimelenga kuwagawa Watanzania.

Kinana amesema hayo jana alipozungumza na wana-CCM wa Mkoa wa Dodoma kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete.

“Sheria ya uchaguzi iliyopo ni nzuri na bora kuliko sheria zilizopita, na muhimu watambue kuwa sheria ya uchaguzi siyo njia pekee ya kushinda, ni lazima uwe na sera nzuri, kukubalika kwa chama na wagombea wanaoteuliwa na kujipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huo ndio mtaji wa ushindi,” amesema.

Kinana ametoa mfano wa nchi jirani bila kuitaja kwamba wamepigania katiba na tume huru ya uchaguzi kwa muda mrefu na wameipata, lakini kuna watu wamegombea mara sita na hawajashinda uchaguzi.

“Sisi hatukatai kukosolewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo,” amesema Kinana.

Kinana amesema hayo kujibu hoja za Chadema kwenye maandamano na mikutano ya hadhara mikoani,  wakitaka Katiba mpya, sheria za uchaguzi, wakieleza maeneo ya nchi kuuzwa kwa sababu Rais ni Mzanzibari na suala la kuondoa mamlaka za mikoa na kuanzisha majimbo.

Amesema suala la Katiba mpya, CCM imelikubali kwa kuwekwa utaratibu, lakini Chadema wamekuwa kikwazo na wameshawahi kujitoa kwenye mazungumzo na CCM, wakitaka wasikilizwe pekee bila vyama vingine vya siasa, wakidai wao ni chama kikuu cha upinzani.

Kinana amesema hata kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria tatu za Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa, na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Chadema walipeleka Bavicha, Bawacha, Bunge la wananchi na uwakilishi wa chama na mawazo yao yalisikilizwa.

Kuhusu hoja ya Chadema kwamba Rais asiwe na mamlaka kwenye tume huru ya uchaguzi, Kinana amesema duniani kote haiko hivyo, kama Rais hateui atakuwa na mamlaka ya kuwaondoa mwenyekiti na makamu mwenyekiti inapokuwa imebidi kufanya hivyo.

Amesema hoja ya Chadema kwamba Zanzibar  wana wabunge wengi wakati idadi yao hawafiki hata watu milioni mbili, haina mashiko kwa sababu kuna nchi nyingi zina idadi ndogo ya wananchi, lakini wabunge ni wengi.

“Kuhoji kwamba Zanzibar yenye watu 1.2 milioni kwa nini wawe na majimbo 71 haina mashiko. Namibia ina watu milioni mbili, lakini wabunge wapo 107, Seychelles ina watu 107,000 lakini wabunge 35, Lesotho ina watu 2.3 milioni lakini wabunge 130. Sasa kusema jimbo la Temeke kuna wapiga kura 300,000 na jimbo moja Zanzibar lina wapiga kura 7,000 si sawasawa,” amesema.

Aponda hoja ya Rais Mzanzibari

Kuhusu Rais Mzanzibari, amesema hilo ni sehemu ya matakwa ya kikatiba na kusema anauza maeneo ya Bara kuliko Zanzibar siyo kweli.

“Kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS), imekuwepo tangu Serikali ya awamu ya tatu, awamu ya nne, awamu tano, awamu ya sita imeiondoa na kuweka DP Word imekuwa tatizo.

“Mkapa (Benjamin Mkapa Rais wa awamu ya tatu) amebinafsisha mashirika zaidi ya 200 alikuwa Mzanzibari? Benki ya NBC (iliyokuwa Benki ya Biashara-NBC), Shirika la Reli lilibinafsishwa kwa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) na ATC (Shirika la Ndege Tanzania), yalibinafsishwa, alikuwa Mzanzibari?” amehoji Kinana.

"Jamaa zetu hawa wanatumia kanuni ya Goebbels (Joseph Goebbels aliyekuwa mkuu wa propaganda wa Serikali ya kinazi ya Ujerumani) ya kusema uongo mara nyingi ili uonekane ni ukweli" amesema Kinana.

"...wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuwa ajenda yao ya uchaguzi kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina Rais Mzanzibari ambaye anataka kuihujumu upande huu wa Bara wa Muungano wanataka Watanzania waaminishwe wajenge chuki juu yao ili iwe ajenda yao ya uchaguzi,” amesema.

"Kwa muda wa wiki kadhaa ndugu zetu wa Chama cha Chadema walipata uhuru mkubwa sana wamefanya maandamano, wamefanya mikutano ya hadhara wamezunguka sehemu mbalimbali nchini wamezungumza mambo mengi," amesema.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa akimkaribisha Kinana kuzungumza na wana-Dodoma amesema mkoa huo wamewakataa wapinzani kwa sababu wanatoa matusi, kejeli na dharau.

"Wananchi wa Dodoma wamekataa upinzani kwa mambo matatu, kwanza Dodoma ni makao makuu ya CCM, pili hawapendi matusi, dharau, kejeli. Tunapenda amani,” amesema.

"Wapinzani wajiongeze kwa kuacha matusi, fujo na wajielekeze kwenye hoja," amesema Kimbisa.

Amesema CCM ndiyo chama imara na kwa Dodoma wananchi wenye migogoro ya ardhi wamekuwa wakikimbilia CCM Bara, ambayo kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri wameweza kupunguza malalamiko ya migogoro ya ardhi.

Lissu ajibu

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amejibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Kinana kuhusu chama hicho ikiwamo ya  Katiba mpya, kupinga sheria ya uchaguzi na muundo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na sera ya majimbo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 5, 2024, Lissu amesema CCM wamekuwa wakipiga danadana suala la Katiba mpya tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992.

“Mwaka 1992 wakati Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipotoa pendekezo la mabadiliko ya Katiba, CCM walisema iwe baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, ikapita, ilipofika 2000, wakasema iwe 2005, ilipofika 2005 wakasema 2010.

“Rais Jakaya Kikwete (mstaafu) alipoleta Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2012, ilipofika 2014 wakasema baada ya uchaguzi wa 2015,” alisema.

“Sasa Rais Samia naye kaingia anasema iwe baada ya uchaguzi wa 2025, nani mwenye akili atakayekubaliana nao?” amehoji.

Kuhusu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Lissu amesema mapendekezo yao kuhusu Katiba na tume huru ya uchaguzi yalikataliwa.

“Ni kweli wamekataa mapendekezo yetu yote. Kimsingi, mapendekezo yetu ni kutaka Katiba ibadilishwe kwa sababu sheria za uchaguzi zinakwenda kinyume cha Katiba,” amesema.

Ametoa mfano wa kuwepo chombo cha uteuzi walichopendekeza, akisema kilichowekwa ni kamati ya usaili.

“Je, kamati ya usaili ipo kwenye Katiba? Hicho walicholeta kinaenda kinyume na Katiba,” alisema na kuogeza:

“Tulisema tume iajiri wafanyakazi wake badala ya kutegemea watumishi wa umma, ambao Rais anaweza kuwatishia kuwafukuza kazi, hiyo wamebadilisha?”

“Tulipendekeza namna ya kupata wajumbe wa tume tukasema ihusishwe tume ya uteuzi, Bunge na Rais, hiyo wametekeleza?”

Ameongeza: “Tulisema katika kutangaza majibu tume itumie uwakilishi sawa, wametekeleza? Tulisema tume iondolewe kinga ya kushitakiwa, imeondolewa kwenye sheria? Tulisema uandikishaji wa wapiga kura uwepo muda wote, ilibadilishwa?’’

Kuhusu maelezo ya Kinana kwamba kwenye kamati ya maridhiano Chadema walitaka wasichanganywe na vyama vingine, Lissu amekiri hilo akidai vyama hivyo ni vibaraka.

“Wale wana shida gani na CCM? Sisi ndiyo wenye malalamiko ni lazima tuzungumze na chama tawala,” amesema.

Kuhusu Muungano, amesema Chadema wamekuwa wakisisitiza muundo wa Serikali tatu.