Kinana kukutanisha vigogo kutatua kero mpaka wa Sirari

Muktasari:

  • Kinana kukutana na Waziri wa Fedha, Mwigulu na Kamshina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kidata kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakuta wananchi kwenye mpaka wa Sirari katika kuvusha bidhaa ndogondogo kutoka nchi jirani ya Kenya.

Mara. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amesema atakwenda kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA, Alphayo Kidata kujadili namna ya kutatua changamoto zinazowakabili  wananchi kwenye mpaka wa Sirari.

Mpaka huo unaounganisha Tanzania na Kenya unalalamikiwa na baadhi ya wananchi kuwa kuna  changamoto ya kuvusha bidhaa,  na wakati mwingine hata wakiruhusiwa  wamekuwa wakitozwa gharama kubwa ikilinganishwa na thamani halisi ya mzigo waliobeba hali inayowaongezea ugumu wa maisha.

Akizungumza jana jioni Jumapili Aprili 14, 2024, katika mkutano wa ndani uliofanyika Tarime Mjini, mkoani Mara, Kinana amesema atakwenda kufanya mazungumzo hayo baada ya kumaliza ziara hiyo, akisema kuwa hakuna haja ya kuwatesa wananchi kama wanapata bidhaa kwa gharama nafuu.

"Hili jambo inabidi nikakae na Waziri wa Fedha na Kamishna wa mamlaka ya mapato ili tuelewane na maagizo yatolewe. Kwa sababu mnaweza kuwa na sera nzuri na msimamo halafu watu walioko pale wakawa hawafuati sheria," amesema Kinana.

Akizungumza changamoto hiyo, Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema kinachofanyika katika mpaka huo bidhaa zinazopatikana Kenya gharama yake ni nafuu, ikilinganishwa na Tanzania.

"Saruji  ukiitaka ya Kenya inakuja hadi nyumba kwako unaipata kwa Sh15,000 hadi Sh17,000 lakini hapa Tanzania Sh25,000 kwa hiyo kama mwananchi wa kawaida lazima atatafuta nafuu.

Amesema wananchi wanachokifanya mpakani wameweka utaratibu wanaofanya biashara za jumla wanaruhusiwa kuingiza bidhaa hizo kwa sababu wamepewa vibali na wanalipa kodi.

"Mwananchi akipitisha bidhaa anakamatwa anaambiwa amepitisha kimagendo, bodaboda wanakamatwa na pikipiki zao kutaifishwa na kupigwa faini," amesema.

Waitara amesema kutokana na urasimu huo umekuwa chachu ya kuwapo kwa rushwa mpakani  hapo, kwani ukitaka urahisi unaelewana na maaskari wapitishe kwa gharama nafuu kwa kufanya mazungumzo ya kificho.

"Tulichoomba sisi na nilishapeleka bungeni waweke utaratibu bidhaa ndogondogo watu walipe kodi ya kawaida ili wapate huduma, lakini kuweka gharama na masharti magumu watu wanaingia uchochoroni na yanakuwa mapambano Serikali inakosa kodi, pia inakuwa na mahusiano mabaya na wananchi wake," amesema Waitara.

Mmoja wa wananchi, Charles Mtatiro ambaye pikipiki yake ilitaifishwa baada ya kukamatwa akivusha mifuko miwili ya sukari kutoka Kenya, amesema wanapitia  wakati mgumu."Hatuoni tija ya kuishi katika mpaka huu, mimi kazi yangu bodaboda walinikamata na wakataifisha pikipiki yangu kila nilipojaribu kufuatilia hawakuwa na habari na mimi, tunakiomba chama kiagize Serikali yake jambo hili hatulipendi na halina haki kwetu," amesema.