Kinana: Serikali iharakishe misaada mafuriko ya Rufiji

Waathirika wa mafuriko Rufiji na Kibiti wakiwa kwenye mkutano uliohutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana leo Aprili 9, 2024. Picha na Tuzo Mapunda

Muktasari:

  • Waathirika wa mafuriko katika Wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani wameomba msaada wa mahitaji muhimu kama chakula na makazi huku watu wawili wakiripotiwa kupoteza maisha.

Pwani. Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana ameitaka Serikali kuharakisha utoaji wa misaada kwa waathirika wa mafuriko yaliyozikumba Wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

Mafuriko hayo yamejitokeza maeneo hayo kutokana na mvua za Masika zinazoendelea kunyesha na kusababisha maji kufurika kwenye makazi na mashamba kuanzia Machi 5, 2024.

Akizungumza leo Aprili 9, 2024 baada ya kutembelea waathirika hao na kusikiliza kero zao, Kinana amesema kiwango cha huduma kinachotolewa hakifanani na shida wanayopitia.

"Maneno mengi sasa hivi hayasaidii, watu wanahitaji huduma za chakula na makazi na ni jukumu la Serikali kuwahudumia wananchi wake.

"Nimekuja kujionea hali halisi na kuwapa pole, najua hata nikiongea hotuba kubwa itakuwa si chochote, naenda kuongea na viongozi wa Serikali," amesema Kinana.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati kiongozi huyo alipotembelea Kata za Mohoro na Chumbi, waathirika hao wameiomba Serikali na wadau kuwasaidia kupata huduma muhimu.

"Kwa sababu mvua zinazoendelea kunyesha na hatujui maji yatapungua lini, tunachohitaji zaidi ni chakula, malazi na huduma za afya," amesema Sifa Hamis, mkazi wa Kitongoji cha Kipoka Kijiji cha Chumbi.

Sifa mwenye watoto sita, amesema wamejihifadhi kwa rafiki yake, lakini bado hawajapata chakula.

Kwa upande wake, Binati Rashid mwenye mtoto mdogo wa mwaka mmoja amesema wanahitaji usalama wa makazi.

"Kwa hali ilivyo kulingana na mvua zinazonyesha, tunaweza kupata magonjwa ya mlipuko. Tumehifadhiwa hapa Shule ya Mahoro lakini unaona maji yanaanza kujaa kwenye baadhi ya madarasa," amesema Binati.

Akitoa taarifa za mafuriko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema hadi sasa athari za mafuriko hayo zimesababisha vifo vya watu wawili katika Kijiji cha Chumbi.

"Watu hao walipoteza maisha wakiwa kwenye boti lilopinduka baada ya kugongwa na magogo, wakiwa kwenye harakati ya kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine," amesema.

Meja Gowele amesema licha ya vifo hivyo kwa tathmini waliyofanya katika kata tisa kati ya 12 jumla ya kaya 23,360 zimeathiriwa.

"Jumla ya watu 88,768 wameathirika na mazao hekta 33,930.24 zimeharibiwa na tunaendelea kufanya jitihada kuwasadia waathirika, ikiwemo kuwapa mazingira ya kuwahifadhi," amesema.