Kiongozi wa Mbio za Mwenge aacha maagizo Mvomero

Kiongozi wa Mbio za Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim (Katikati) akizungumza jambo na Ofisa Mifugo Mwandamizi wilaya ya Mvomero, Hassan Rupindo wakati mbio za Mwenge wa Uhuru ilipozindua Mradi wa shamba la malisho ya mifugo la Shambakubwa Longido wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, (kushoto) ni Mkuu wa wilaya hiyo, Judith Nguli. Picha na Juma Mtanda.

Muktasari:

  • Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 umezindua mradi wa shamba la nyasi la mfugaji Shambakubwa Longido kwa ajili ya kulisha mifugo hasa nyakati za kiangazi ambapo ndio kipindi kikame.

Morogoro. Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023 ameutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero kuendelea kutoa elimu ya kutunza vyanzo vya maji na ufugaji wa kisasa pamoja na kilimo ili jamii ya wafugaji na wakulima kuondokana na migogoro inayoleta athari na kuathiri maendeleo mkoani hapa.

 Akizungumza kuzindua na kupitia jumla ya miradi nane yenye thamani ya Sh1.174 bilioni leo Mei 13, 2023 wilayani hapa, Kiongozi huyo wa Mbio za Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim amesema viongozi wana jukumu la kuendelea kutoa elimu katika sekta ya mifugo na kilimo ili jamii ya wafugaji na wakulima waheshimiane katika shughuli zao za kujipatia kipato.

Shaibu amesema wafugaji wawaheshimu wakulima na wakulima nao wawaheshimu wafugaji hasa kuepuka kuingiliana katika shughuli zao za kiuchumi kwa makundi hayo kuendelea kutunza vyanzo vya maji kwani wamekuwa wakiharibu mazingira na makundi hayo yamekuwa moja ya vyanzo vya uhalibifu kwa shughuli za kulima na ufugaji lakini muingiliano wao huzalisha migogoro inayopelekea kuleta athari za kimaendeleo.

“Jamii za wafugaji na wakulima waheshimiane kwa kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima kwa mfugaji asifanye shughuli za kiufugaji kwa kupeleka mifugo kwenye vyanzo vya maji na wakulima wasilime ndani ya mita 60 iliyozuiliwa hivyo makundi hayo yanapaswa kuheshimiana na viongozi wana jukumu la kutoa elimu zaidi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji na kuharibu vyanzo vya maji,”amesema Shaibu.

Meneja Misitu Wilaya ya Mvomero, Michael Kimata amesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilaya hiyo imetoa miche zaidi ya 100,000 iliyopelekwa kwa makundi mbalimbali na kupandwa kama sehemu ya kurejesha uoto wa asili ulioharibifu kutokana na shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji na kuharibu misitu.

“TFS imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inatunza misitu na wadau wengine ili kupambana na makundi machache yanayoharibu mazingira wakiwemo wafugaji na wakulima kuharibu vyanzo vya maji na ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2023 wa Mabadiliko ya Tabianchi, Hifadhi ya Mazingira na Utunzaji wa Nyanzo vya Maji na Mvomero tunapaswa kuunga juhudi za ujumbe huo ili kunusuru uharibifu unaofanyika lakini kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Michael.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Judith Nguli alisema Mwenge huo umezindua na kupitiwa na miradi nane yenye thamani ya Sh1.174 bilioni.

“Miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni pamoja na ujenzi wa barabara kiwango cha lami Dakawa - Kibaoni (0.8 km), Ujenzi wa bwawa la samaki katika Kituo cha Mafunzo ya Wakulima na wafugaji Kijiji cha Wami Sokoine, Ufunguzi wa matumizi ya X-ray katika Hospitali ya Wilaya, ujenzi wa Kituo cha Ufundi wa Awali, Mradi wa Shamba la Malisho ya Mifugo linalomilikiwa na Shambakubwa Longido,  Mradi wa  Kikundi cha Vijana “Youth Vibrated Block” Mradi wa Utunzaji wa Vyanzo vya Maji na Ujenzi wa Madarasa nane ya Shule ya Sekondari Kipera,”alisema Judith.