Kipindupindu chaua Mzee wa miaka 99 Geita, 12 wagonjwa

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema wagonjwa  wa kipindupindu mkoani humo wamefikia 12.

Geita. Hali ya ugonjwa wa kipindupindu katika Mkoa wa Geita inazidi kushika kasi, baada ya wagonjwa 12 kubainika kuugua ugonjwa huo huku mmoja akipoteza maisha.

Kwa mujibu wa Serikali mkoani humo, aliyepoteza maisha ni Mzee mwenye umri wa miaka 99, mkazi wa Masumbwe wilayani Mbogwe mkoani Geita ambaye jina lake halikuwekwa wazi.

Taarifa kuhusu wagonjwa hao, imetolewa leo Jumatatu, Januari 15, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella alipozungumza katika kikao cha wadau wa sekta ya afya ngazi ya Mkoa kilichokuwa kikijadili mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo.

Ameeleza kati ya wagonjwa hao, tisa wanatoka katika Wilaya ya Mbogwe na watatu kutoka katika Wilaya ya Chato.

Hata hivyo, amesema udhibiti umeendelea kufanyika kuhakikisha ugonjwa huo hauendelei kuenea na kwamba kwa jana hakuna mgonjwa aliyepokelewa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Omari Sukari amesema mgonjwa wa kwanza aliripotiwa kwenye mji mdogo wa Masumbwe wilayani Mbogwe na uchunguzi  ulibaini chanzo cha ugonjwa huo ni matumizi ya maji yasiyo salama.

“Alianza kuugua dada wa kazi alifika hospitali na kupata matibabu alikua akiharisha na kutapika lakini kesho yake kwenye familia hiyohiyo walikuja wengine watatu akiwemo huyo mzee aliyepoteza maisha.

“Tulipima visima vitano vya eneo hili na viwili kati ya hivyo tulibaini uwepo wa vimelea na kimoja kilikua mita nane kutoka kwenye choo wanachotumia na tukabaini ugonjwa waliopata umetokana na maji yasiyo salama kitaalam kisima cha maji kinapaswa kuwa mita 30 hadi 50, kutoka kwenye choo,” amesema.

Dk Sukari amesema kesi nyingi za kipindupindu zinatokana na ukosefu wa vyoo na takwimu zilizofanywa kwenye kaya 3,000 zilizopo Masumbwe wilayani Mbogwe zinaonyesha familia 418 kati ya hizo hazikuwa na vyoo kabisa.

Mratibu wa huduma za matibabu Mkoa wa Geita, Dk Yohane Kihaga amesema jamii inapaswa kuwa na vyoo bora na wale wenye vyoo vya shimo wanapaswa kuvifunika wakati wote.

Amesema uchemshaji wa maji ya kunywa ni muhimu kwa kuwa mengi yanayotumika si salama.