Kitita cha matibabu chawaibua madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akifungua mkutano wa Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Ndani Tanzania (APHYTA), jijini Dar es Salaam, leo Mei 2, 2024.

Muktasari:

  • Washauri Serikali kutoa kipaumbele kwenye huduma za matibabu zinazotolewa, Waziri wa Afya, yataka mapendekezo

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kufanyia maboresho sekta ya afya ikiwamo kuimarisha matibabu kwa kuweka vitita kwa wagonjwa wanaotibiwa kwa bima, Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Ndani Tanzania (APHYTA) kimeshauri maboresho hayo yasiathiri ubora wa huduma.

Ushauri huo umetolewa kutokana na maboresho yaliyofanyika hivi karibuni ya kitita cha matibabu kilicholalamikiwa na baadhi ya watoa huduma za afya kwa kile kinachoelezwa hakiendani na uhalisia.

Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya vituo binafsi vya afya kusitisha utoaji huduma kwa wagonjwa wanaotibiwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kati ya Machi 1 na 2, 2024 kabla ya kurudisha tena huduma.

Akizungumza leo Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa APHYTA , Rais wa chama hicho, Dk Mwanaada Kilima amesema kutokana na mabadiliko ya kisayansi tafiti nyingi zinafanyika na kuzalisha huduma mpya za matibabu, na vipimo ambavyo havijaingizwa kwenye kitita kipya.

“Kwetu sisi namna kitita cha bima yoyote kinavyoweza kutoa huduma ndivyo tunavyoweza kutoa huduma bora, kwa sababu kitita kinaathiri ubora wa huduma. Ninavyosema haya sina maana kwamba kitita hakiendani na mwongozo ila kuna maboresho ya hapa na pale yanapaswa kufanyika,” amesema Dk Kilima.

“Mimi nikiwa kama mtaalamu ninayemhudumia mgonjwa sijisikii vyema pale ninaposhindwa kumpatia matibabu anayostahili kwa sababu kitita chake hakiruhusu kupata huduma hiyo. Wito wetu kwa mashirika ya bima kuja na vitita ambavyo vitawezesha watu kupata huduma bila kuathiri ubora.”

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliyefungua mkutano huo amewataka watalaamu hao kutoa mapendekezo kwa kuzingatia Mwongozo wa Taifa wa Matibabu na Orodha ya Taifa ya Dawa.

“Hatuwezi kuendesha sekta ya afya shaghalabaghala lazima tuwe na mwongozo wa utoaji wa huduma za matibabu, mnachotakiwa kufanya kama wanataaluma leteni maoni yenu kwenye mwongozo wa Taifa wa matibabu na orodha ya Taifa ya dawa muhimu,” amesema Waziri Ummy.

“Kusanyeni maoni yote ya chama halafu leteni mapendekezo yenu, kwa sasa niwaeleze kuwa suala la kitita cha NHIF linatakiwa lijadiliwe kwa kufuata mwongozo wa matibabu na orodha ya dawa. Kitu kingine muhimu tuelewe NHIF haiwezi kutoa huduma bila kikomo, hatuwezi kuingiza dawa za dunia nzima tutaangalia zile muhimu si brand.”

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amewataka wataalamu hao kuomba fursa za masomo za kuongeza ujuzi katika ngazi ya ubobezi na wawe tayari pia kufanya kazi katika maeneo ya pembezoni.

“Huwa zinatoka fursa za masomo ombeni mkaongeze ujuzi na mkimaliza msing’ang’anie kubaki Dar es Salaam, kwa sababu madaktari wa magonjwa ya ndani mnahitajika kila mahali hata watu wa pembezoni wanahitaji huduma zenu. Kama hamuwezi kwenda huko, basi tufikirie kuwapa kipaumbele wale ambao wako tayari mikoani,” amesema Waziri Ummy.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Elisha Osati amesema hatua kubwa imeendelea kupigwa katika uboreshaji huduma za matibabu nchini hali inayowarahisishia utendaji kazi wao ingawa amesisitiza bado jitihada zinapaswa kuwekwa kwenye eneo la huduma za maabara.

“Tunashuhudia maboresho ya hali ya juu kuanzia kwenye miundombinu, vifaatiba, kuongeza idadi ya watoa huduma na maboresho kwenye huduma za uchunguzi, naweza kusema tunapiga hatua na inatusaidia sisi watoa huduma,” amesema.

“Changamoto bado tunaiona kwenye huduma za maabara, si kwamba tupo palepale ila kuna mengi bado hayajafanyika hali inayosababisha hadi sasa kuwepo na sampuli ambazo zinapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kuchunguzwa,” amesema Osati.

Amezitaja vipimo hivyo ni vile vinavyohusisha uchunguzi wa vinasaba na baadhi ya sampuli zinazochukuliwa kwa wagonjwa wanaopandikizwa figo.

Dk Osati amesema changamoto hiyo wakati mwingine inasababishwa na kukosekana kwa mashine za kupima sampuli hizo hapa nchini, ukosefu wa wataalamu wabobezi wa kuchunguza sampuli husika au vitendanishi, hivyo uwekezaji mkubwa unapswa kufanyika pia katika eneo hilo.