Leseni za madini sasa kulipiwa kwa mtandao

Muktasari:

Alisema utawawezesha pia wateja kupata ramani za kijiolojia, takwimu mbalimbali za madini na kufanya malipo kwa njia ya miamala ya simu za mkononi, Maxmalipo na kupitia benki (EFT).

Dar es Salaam. Wizara ya Nishati na Madini, imezindua matumizi ya mfumo mpya wa malipo ya ada za leseni za madini kwa njia ya kielektroniki (OMCTP)

Kaimu Kamishna Mkuu wa Madini, John Nayopa jana alisema mfumo huo ulianza kutumika wiki iliyopita na utawawezesha wateja kutuma maombi ya leseni na taarifa za utendaji kazi kwa njia ya mtandao.

“Mfumo huu ni salama kwa fedha za wateja na kuanzia sasa malipo ya ada za leseni yatafanyika kwa njia ya mtandao pekee. Ofisi zetu za madini zitatoa msaada kwa wateja wanaohitaji maelekezo,” alisema.

Alisema utawawezesha pia wateja kupata ramani za kijiolojia, takwimu mbalimbali za madini na kufanya malipo kwa njia ya miamala ya simu za mkononi, Maxmalipo na kupitia benki (EFT).

Nayopa amewataka wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya madini na kuchakata mchanga wenye madini ili wanufaike na Serikali iongeze mapato kwa kupitia ulipaji wa kodi.

Mfumo huo unalenga kurahisisha utoaji wa leseni wachimbaji wadogo, kupunguza mlundikano wa maombi ofisi za madini, kurahisisha mawasiliano kati ya wizara na wamiliki, kujua taarifa za leseni na utoaji wa taarifa za madini kwa wakati