Lissu afunguka wanaohoji kauli yake kuhusu rushwa Chadema

Muktasari:

  • Lissu amesema kuwa alitoa kauli hadharani kwamba kuna fedha za rushwa zimemwagwa kwenye chama hicho, kwa sababu rushwa ni tatizo kubwa kwenye siasa linalohitaji kukemewa ndani na nje ya vikao.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu ameeleza kushangazwa kwake na baadhi ya wanachama na wapenzi wa chama hicho wanaohoji kauli yake ya kupinga rushwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa Mei 2, 2024, Lissu alisema kuna fedha zimemwagwa na kwamba zinaweza kuharibu uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

“Wakati nakuja hapa Iringa jana na juzi kulikuwa na mtafaruku mkubwa sana, sijui kama mnafahamu, ndani ya chama chetu kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu,” alisema Lissu.

Lissu aliwaonya wanachama wa chama hicho kujiepusha na fedha za rushwa ili kukinusuru chama hicho.

Kauli hiyo ya Lissu imezua mjadala miongoni mwa makada wa Chadema, wakihofu kutokea mvutano kati ya Lissu na viongozi wa juu wa chama hicho.

Juzi Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni alisema watafuatilia taarifa zozote za kuwepo rushwa ndani ya chama hicho.

Jana Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema atatoa kauli juu ya kilichosemwa na Lissu baada ya vikao vya chama hicho.

Akizungumza leo Mei 5, 2024 katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital, Lissu amesema alitoa kauli hiyo kwa sababu rushwa ni tatizo kubwa kwenye siasa linalohitaji kukemewa ndani na nje ya vikao.

“Rushwa ni miongoni mwa mambo yanayoharibu nchi na yanahitaji kukemewa na kila mtu.”

“Kuna kitu kinanishangaza, kwa nini watu wanasema tuzungumzie ndani? Tangu lini imekuwa kosa kuzungumzia rushwa hadharani?” amehoji.

Amesema suala hilo si kwa Chadema peke yake, bali hata CCM wamekuwa wakikemea.

“Mwalimu (Julius) Nyerere alikemea rusha mpaka akaandika kitabu cha Nyufa. Kuna mtu alikemea rushwa hadharani kama Nyerere,”Lissu amesema na kuhoji.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kuwepo kwa mvutano kati yake na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na pengine ana mpango wa kugombea uenyekiti wa chama hicho, Lissu amekanusha.

“Mimi sina mpango wa kugombea uenyekiti wa Chadema. Kwa miaka minane nimekuwa nikisema hivyo, mnataka niseme mara ngapi? Watu wanaosema hayo ni wajinga.”

“Hayo maneno yalikuwepo tangu mwaka 2007 wakati wa Chacha Wangwe. Mwaka 2017 nilipopigwa risasi wakasema Mbowe ndio amenipiga kwa sababu nataka uenyekiti,” amesema.

Alipoulizwa kama kauli yake haiwezi kukinzana na katiba ya chama hicho inayotakiwa kutowatuhumu viongozi wenzake hadharani. Lissu  amehoji, “Nimemtaja nani? Nimesema kuna hela zimemwagwa na sina uhakika ni za nani.

“Ajabu ni kwamba kuna watu hawataki tuzungumzie rushwa hadharani,” amesema.

Alipoulizwa kama amehojiwa na viongozi wenzake kuhusu kauli hiyo, amejibu: “Nihojiwe kwa kosa gani?

Amesema kauli kama hizo pia zimetolewa hadharani na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alipokuwa akifungua uchaguzi wa jimbo la Kawe Dar es Salaam hivi karibuni.

“Mnyika naye alitoa maneno hayohayo, alikemea rushwa kwenye uchaguzi.”

Kauli ya Lissu imekuja wakati kukiwa na mchuano mkali kati ya Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi (Sugu) wanaowania uenyekiti wa Kanda ya Nyasa.

Mei 2, 2024  wakati Lissu akihutubia mkutano wa hadhara Iringa, alisema awali kuna watu walitaka asiende kwenye mkutano huo. Alipoulizwa ni kina nani waliokuwa wakimzuia amesema alitumiwa meseji na vijana wa chama.

“Nilitumiwa meseji nyingi tu na vijana, nikawapigia simu nikawauliza shida nini? Wakasema nakwenda kumpigia kampeni Msigwa, nikawaambia siwezi kumpigia kampeni, kwa sababu yeye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, kama mna hofu njooni,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kumuunga mkono Msigwa, amekanusha.

“Mimi sina kambi, kambi yangu ni Chadema. Wapo watu wanajitangaza mitandaoni mwetu wanaweka wazi kabisa kwamba wanamuunga mkono nani. Mimi sijajitangaza kwa sababu najua itakuwa ni rushwa.

“Watu wanasema mimi ni rafiki wa Msigwa, ni kweli na mimi ni rafiki wa Sugu (Joseph Mbilinyi). Hawa ni rafiki zangu kwa miaka mingi, nimefanya nao kazi, hata kuna wakati niliwaalika kwenye jimbo langu wakanisaidia kampeni.”

Kuhusu kugombea urais mwaka 2025, Lissu amesema ni mpaka chama kimteue.

“Kama wataniteua ni sawa tu na wasiponiteua ni sawa, mimi sikuzaliwa kuwa mgombea urais. Mwaka 2020 niligombea baada ya wanachama kuona ninafaa,” amesema.

Kuhusu hatari ya chama hicho kuingia kwenye mgogoro Lissu alisema hafikiri kufika huko.

“Mimi sijapanga mapinduzi, wala sijatengeneza wana mtandao.”