Lusinde awashukia bungeni wanaomtusi Rais Samia mitandaoni

Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde akizungumza wakati akichangia makadirio ya mpato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25 leo Jumatano Aprili 17, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

Mbunge wa Meatu, Leah Komanya amesema mtu wenye matunda ndiyo hupigwa mawe.

Dodoma. Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde amesema bungeni akisema wanaomtusi Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mitandao ya kijamii wanajipotezea muda bure.

Lusinde amesema hayo leo Jumatano Aprili 17, 2024 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25.

Amesema kuna wachambuzi wengine wanalalamika kwa nini Rais Samia anatajwa sana, lakini soka huwa wanaotajwa sana ni wale wenye kumiliki mpira.

“Rais Samia anamiliki mpira wa maendeleo na ndiyo maana tunamtaja sana, wewe itakuwaje tu unasema wanaenda Yanga, unasema wanaenda Simba, anaenda Chama. Sisi tumekaa hapa miaka 15, hatujaona Serikali ikishusha pesa kama anavyofanya Rais Samia,” amesema.

Amesema hayo yote yanayotokea, Watanzania waendelee kumwombea Rais Samia awe na moyo wa subira na uvumilivu.

Lusinde amesema, “kwa sababu tunaotukanwa ni sisi sote, tunamwambia wako pamoja naye katika shida na raha na wameamua kwenda naye.” 

“Tunaona Mtume (S.A.W), kiongozi wa dini ya Kiislamu alivyopata shida, ukimwangalia Yesu naye alipigwa. Rais Samia ni nani asiyapitie hayo na yeye ni binadamu? Kwa kazi anazozifanya baadhi ya watu watamzushia mambo mengi?” amesema.

“Nawaambia wanapoteza muda bure. Rais tutaendelea kumwombea na kumpigania. Kwamba shida anayopitia ni kwa ajili yetu, kwa hiyo hayuko pekee yake, tuko pamoja naye,” amesema.

Akiguzia hilo, Mbunge wa Meatu, Leah Komanya amempongeza Rais Samia kwa maendeleo anayowapatia, akisema katika kipindi cha miaka mitatu amefanya mabadiliko makubwa katika jimbo lake.

Amesema wako pamoja naye na kwa kawaida mti wenye matunda mazuri ndiyo hushambuliwa kwa mawe.

“Kwa hiyo haya yote yanafanyika kwako (Rais) kwa sababu ya kazi nzuri unayoifanya. Wanataka wakudhoofishe urudi nyuma na mimi kama mbunge wa Meatu nakutia moyo, uko vizuri na tuko pamoja katika yote unayopitia,” amesema.

Aprili 15, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akiwa katika kumbukizi ya miaka 40 tangu kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Sokoine, alidai anawafahamu baadhi ya watu wanaotuma watu kumchafua Rais Samia mitandaoni, wakiwemo mawaziri.

Alisema endapo hawangeacha kufikia Aprili 15, 2024 angewataja kwa majina. Hata hivyo, leo ikiwa ni sikumbi baadaye hajamtaja yeyote.

Hata hivyo, Aprili 15, 2024 Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Serikali haitakuwa na “simile wala mswalie Mtume” kwa yeyote atakayebainika kumchafua Rais mtandaoni.

Masauni alisema hayo alipozungumzia mafanikio yaliyopatikana kwenye wizara hiyo kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.