Madaktari bingwa 15 kutua Mbeya, kuchunguza saratani kwa wanawake

Mratibu wa huduma za afya ngazi ya jamii kutoka shirika la HJFMRI, Dk Constantine Ntanguligwa akizungumza na waandishi wa habari  leo Mei 7,2024. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Katika hatua ya upimaji, madaktari bingwa hao na wabobezi kutoka hospitali za rufaa ngazi za mikoa, watatoa pia huduma ya ushauri kwa wanawake na jamii itakayo jitokeza bure kwa siku mbili.

Mbeya. Madaktari bingwa 15 wanatarajiwa kuwafanyia uchunguzi wa saratani wanawake zaidi ya 1,000 jijini hapa wakati wa Tamasha la ‘Usiku wa Mama’ litakalofanyika Mei 14, 2024 huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

 Mbali na saratani, pia huduma ya kupima Virusi vya Ukimwi (VVU), itatolewa siku hiyo ambayo itakuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani.

Imeelezwa kuwa hatua hiyo imelenga kuwahamasisha wanawake kupima afya zao baada ya takwimu kuonesha  asilimia 74 ya  Watanzania nchini wako hatarini  kupoteza maisha kutokana na  magonjwa yasiyoambukiza huku wanawake wakionekana wako katika hatari zaidi.

Takwimu hizo zilitolewa hivi karibuni na Naibu Msajili wa Bodi ya Maabara Binafsi kutoka Wizara ya Afya, Naomi Mkingule mkoani hapa.

Akizungumzia leo Jumanne Mei 7, 2024, na Mwananchi Digital, Mratibu wa  Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Shirika la HJFMRI, Dk Costantine Ntanguligwa amesema mbali ya huduma ya upimaji wa saratani kwa wanawake, watatoa pia huduma ya upimaji wa VVU kwa kundi la vijana na wale wa rika balehe.

Amesema katika hatua ya upimaji, madaktari bingwa hao na wabobezi kutoka hosptali za rufaa ngazi za mikoa, watatoa pia huduma ya ushauri kwa wanawake na jamii itakayojitokeza bure kwa siku mbili.

"HJFMRI tunashirikiana na Serikali kupitia  hospitali za mikoa na halmashauri, lengo tunataka kuhakikisha kuna uwepo wa vifaa tiba na kinga dhidi ya maambukizi ya VVU kwa makundi ya vijana na rika balehe ili  kupunguza maambukizi ifikie alama 95 tatu,” amesema Dk Ntanguligwa.

Muandaaji wa tamasha hilo, Edwin Luvanda kwa kupitia kampuni yake ya Branding & Entertaiment, amesema wataanza upimaji huo Mei 12 ,2024 katika Viwanja vya Chuo cha Uhasibu (TIA).

Amesema Mei 14, 2024 ambayo ni kilele cha Siku ya Mama Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera atazindua rasmi upimaji huo na mgeni rasmi atakuwa Waziri Ummy.

"Kwa maana hiyo, Mei 12 tunaanza na tamasha la michezo mbalimbali, kutakuwa na mashindano ya kukimbia ya wanawake wanene na wembamba sambamba na upimaji wa afya kwa magonjwa ya saratani,” amesema Luvanda.

Mdau wa Masuala ya Afya, James Majeba amesema kutokana na takwimu zilivyo kuna haja kwa wadau kuungana na Serikali katika kutoa elimu kwa watu wajue namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambikiza.

“Kuna ugonjwa mwingine mtu anaweza kuuepuka kirahisi kabisa, ila kwa kuwa hatujui, tunajikuta tu tunaumwa, nadhani elimu inahitajika zaidi,” amesema.