Madereva Tanga – Horohoro wagoma, kisa hiki hapa

Kaimu mkuu wa Usalama Barabarani wilaya ya Tanga, Rajabu Ngumbi akizungumza na na madereva wa mabasi ya Tanga- Holoholo ambao wamegoma kuendelea na safari  ili kutafuta ufumbuzi wa suala la nauli. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Madereva na wapiga debe hao wanagomea nauli iliyopangwa na Latra ya Sh3,200 Kwenda Horohoro badala yake wanataka iwe Sh3,500 na kwa abiria wa Maramba iendelee kuwa Sh4,000.

Tanga. Madereva wanaofanya safari zao kutoka Tanga Mjini kwenda wilaya ya Mkinga eneo la Horohoro ulipo mpaka wa Tanzania na Kenya, wamegoma kusafirisha abiria kutokana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) kushusha nauli huku bei ya mafuta ikiwa imepanda.

Akizungumza katika Stendi ya Mwembe Mawazo ulipofanyika mgomo huo, leo Mei 2, 2024, Makamu mwenyekiti wa stendi hiyo, Mohamedi Chiya amesema sababu ni kushuka kwa nauli.

Katika kauli hizo, wanadai Latra inataka abiria kutoka Tanga hadi Holoholo walipe Sh3, 200 huku wao wakitaka Sh3,500.

Amesema nauli ya Sh3, 200 kwao haina faida na kuwa imengwa wakati bei ya mafuta ikiwa imepanda, hivyo kwa kuwa abiria wenyewe wamekubali nauli ya Sh3, 500, magari yaachwe yaendelee nayo.

Sababu nyingine ya mgomo huo, amesema ni kutozwa faini na Latra kwa makosa ya kuzidisha nauli bila kufuatilia na kupata ushahidi

“Wakipata taarifa kutoka kwa abiria, wao wanaandika faini kwa gari husika, jambo ambalo linawaumiza,” amesema Chiya.

Tunataka nauli iwe ileile, kutoka Tanga kwenda Horohoro Sh3,500 na kutoka Maramba kuja Tanga ibaki Sh4,000 kwa sababu mafuta na vipuri vya magari vimepanda,” amesema Chiya.

Abiria anayetumia njia hiyo, Mamgaya Mbega amesema wapo tayari kulipa nauli ambayo imepangwa, kwa sababu kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara gharama za usafiri, hali ambayo imekuwa ikisababisha mgogoro kati ya Latra na madereva.

Amesema ili abiria wasiathirike na migomo ya mara kwa mara, mafuta yakipanda, nauli pia zipande, lakini ikitokea mafuta yanashuka basi Latra waangalie upya utaratibu wa nauli.

Abiria mwingine, Fatuma Rajabu ameitaka Latra kukaa pamoja na madereva kabla ya kupandisha nauli ili kama kuna changamoto wazimalize kwanza badala ya kufanya uamuzi wenyewe bila kushirikisha wadau wao na baadaye kutokea mgomo.

 Ofisa Mfawidhi wa Latra mkoa wa Tanga, Shadrack Malale amesema kwa viwango vyao, kwenda Holoholo kutoka Tanga mjini, nauli ni Sh3, 200 lakini wasafirishaji wanatoza Sh3,500 wakidai chenji ndio inasumbua.

“Kuna abiria wanaridhika na nauli ya Sh3,500 na wengine hawaridhiki, hivyo ni hekima tu itumike kwa yule ambaye analipa Sh3,200 apokelewe na kama kuna haja ya kurudishiwa chenji ifanyike hivyo kama sheria inavyoelekeza,” amesema Malale.

Kaimu mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Tanga, Rajabu Ngumbi amesema wameshazungumza na viongozi wa madereva hao kwa kushirikiana na Latra kumaliza mgogoro huo na muda wowote magari yangeanza safari.

Hata hivyo, baadhi magari yameonekana kuanza kupakia abiria, baada ya kikao cha awali baina ya viongozi wa stendi,Latra na Polisi.