Madereva waendelea kulalamika foleni mpakani Tunduma

Muktasari:

  • Madereva wa malori ya mizigo katika mpaka wa Tunduma, mkoani Songwe, wamelalamika kukaa zaidi ya siku kumi mpaka wa Tunduma, wakisubiri kuvuka kwenda Zambia.

Songwe. Madereva wa malori ya mizigo katika mpaka wa Tunduma, mkoani Songwe, wamelalamika kukaa zaidi ya siku kumi mpakani Tunduma huku wakisubiri kuvuka kwenda Zambia.

Madereva walitoa malalamiko hayo katika kikao chao na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael, aliyekutana nao kusikiliza changamoto wanazopitia.

Mmoja wa madereva Peter George, amesema yupo hapo mpakani kwa siku ya 12 sasa, huku akieleza kuna hujuma zinazofanywa na watumishi kupitisha magari madogo yakiwa yamebeba mizigo kwa kuyasindikiza huku wakiwaacha wenye malori kwenye foleni.

“Mimi nipo pale kichangani, inapofika saa sita kwenda saa saba, utaona kuna gari inakuja inashuka ikiwa na mzigo mzito, huku gari za tenki za mafuta zikifuata nyuma, watu wamechoka,” amesema George.

Halfani amesema Kasumuli ni mpaka mdogo lakini unapofika pale unachukua karatasi unamkabidhi wakala anapeleka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), unaingia upande wa Malawi nako unakaa saa tatu hadi nne unaondoka.

“Kwa nini hilo hapa Tunduma linashindikana, kuna mzizi gani, gari lenye mafuta linakaa siku tano na nyaraka zimetoka!” alihoji dereva huyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Dk Francis Michael, amesema Serikali imeliona tatizo hilo, na mkandarasi anayetakiwa kujenga barabara nne katika eneo hilo ameshafika ofisini kwake tayari kuanza kazi ambapo kukamilika kwake kutasaidia kuondoa tatizo hilo.