Madiwani Mbeya Vijijini walia ubovu, uchakavu wa miundombinu

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mbeya Vijijini wakiwa katika kikao cha robo tatu ya mwaka leo Mei 10,2024. 

Muktasari:

  • Kikao cha baraza hilo kilikuwa cha robo tatu ya mwaka, ambapo hoja ya miundombinu ya barabara ilionekana kutawala zaidi kila mmoja akielezea changamoto katika maeneo yake.

Mbeya. Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Mbeya Vijijini wameiangukia Serikali kuomba kujengewa miundombinu mibovu na chakavu ya barabara na umeme, ambayo imekuwa ikisababisha kero kwa wananchi wilayani humo.

Wakizungumza leo Mei 10, 2024 wakati wa Baraza la Madiwani katika halmashauri hiyo, madiwani hao wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiwasilisha kilio hicho, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Madiwani hao wamewawakia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wilayani humo kumaliza changamoto ya uchakavu wa miundombinu hiyo ya barabara.

Diwani wa kata ya Ihango, Haustine Mwandile amewaangukia Tarura kumaliza kilio cha wananchi wanaoteseka kutumia daraja la Gwaziba lililopo katika Mto Gwaziba linalodaiwa kuua watu 12.

Amesema wananchi katika kata hiyo wamejawa na hofu kutokana na kupoteza ndugu, jamaa na marafiki zao huku akieleza kuwa hivi karibuni gari nalo lilisombwa na maji katika mto huo.

“Ni muda mrefu nawasilisha kero hii lakini naahidiwa kila mara bila hatua kuchukuliwa hatua, sasa naomba Tarura mko hapa nipeni majibu ni lini daraja hili linalounganisha vijiji vya Ilea na Gwanzilo wilayani Chunya litakamilika ili wananchi warejeshe matumaini.

“Hadi sasa jumla ya watu 12 wamepoteza maisha  mwishoni mwa mwaka jana wakivuka eneo lile, naomba kupata uhakika ili amani ya wananchi pale kwenye kata yangu waweze irejee,” amesema Mwandila.

Kwa upande wake, diwani wa kata ya Itewe, Moshi Raphael amesema changamoto za barabara zimekuwa shida hasa kipindi hiki cha mvua nyingi akiomba kuwepo kwa mkakati wa kutatua kero hiyo.

“Hata katika kata yangu, kero ya barabara ni kubwa, niliomba kuwepo hata changarawe ili iweze kupitika kirahisi, changamoto ni kubwa,” amesema Raphael.

Kilio hicho kilikuwa sawa na cha diwani wa kata ya Swaya, Julius Ntokani aliyeomba kuwepo barabara rafiki katika maeneo yake ili kumaliza changamoto kwa wananchi.

Naye diwani wa kata ya Iziwa, Abel Mazembe amesema licha ya umeme kufika katika kijiji cha Iwiji katani humo, bado wananchi hawajanufaika kutokana na Shirika la Umeme (Tanesco) wilayani humo, kutowasha huduma hiyo ikiwemo kwenye taasisi za umma.

“Pamoja na kwamba umeme umefika lakini hatujanufaika nao tunaona nguzo peke yake, haujawashwa ili tunufaike nao, hivyo niombe kuwapo juhudi ili kufikia malengo,” amesema Mazembe.

Akijibu kero za daraja hilo, Mageuzi Mathew aliyemuwakilisha Meneja wa Tarura wilayani humo, Boniface Kasambo amesema ujenzi wa daraja hilo kwa sasa upo Tanroads na mchakato wake umefikia hatua ya manunuzi na bajeti yake imepangwa katika mwaka wa fedha 2024/25.

“Kwa mwaka wa fedha unaoisha 2023/24, Tarura Wilaya ya Mbeya Vijijini tulipata zaidi ya Sh3.11 bilioni, ambapo tunaendelea kurekebisha barabara zote zilizo chini yetu, mengine siwezi kuahidi bali nitawasilisha kwa Meneja ili kikao kijacho aweze kutoa maelekezo,” amesema na kuongeza:

“Lakini zipo pesa za dharura tumeomba kwa ajili ya kukamilisha maneno korofi, hivyo diwani yeyote mwenye changamoto zaidi aje ofisini tushauriane,” amesema Mathew.

Naye mratibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Esau Novath amesema hadi sasa wamefikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 132 kati ya 140 na vinane vilivyobaki vimewekwa katika mpango wa Serikali kuhakikisha vinapata nishati hiyo.

“Halmashauri yetu (Mbeya Vijijini) ina vijiji 140 ambapo hadi sasa ni vinane ndio havijafikiwa na vimewekwa katika mpango wa Serikali, lakini kwa vitongoji 935 ni 357 ambavyo havijafikiwa na nishati hii na tunaamini kufikia Juni 15 tutawafikia,” amesema Novath.

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mwalingo Kasemba amewataka madiwani wote kufanya tathmini binafsi ya kila mmoja kuona alichokifanya kwa kipindi cha miaka minne,  pamoja na kupata takwimu za miradi ya maendeleo iliyotekelezwa pamoja na gharama yake katika maeneo yao.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Paul Sweya amewaomba madiwani kutoa ushirikiano katika makusanyo ya mapato ili kusaidia uendeshaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.