Magufuli mgeni rasmi mkutano mkuu Jumuiya ya Waislamu ya Ahmadiyya

Muktasari:

Jumuiya ya Waislamu ya Ahmadiyya itafanya mkutano wake mkuu kuanzia Septemba 27 hadi 29, 2019 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Joseph Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa miaka 50 wa Jumuiya ya Waislamu ya Ahmadiyya uliopangwa kuanza Ijumaa Septemba 27 mpaka Septemba 29 eneo la Kutonga, Kata ya Msongola jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 25, 2019 Mbashir Mkuu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh  Tahir Mahmood Chaudhry amesema mbali ya Rais Magufuli, pia viongozi mbalimbali wa dini na mabalozi  wamealikwa katika mkutano huo ambao maada kuu itakuwa ni Ibada.

Sheikh Chaudhry amesema mkutano huo umepangwa kuanza saa 7 mchana na utashirikisha washiriki zaidi ya 6,000 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema kuna washiriki kutoka nchi  za Kenya, Pakistan, Uganda, Burundi, Malawi na Msumbiji.

Amesema jumla ya mambo nane yatajadiliwa katika mkutano huo ikiwa pamoja na elimu, misingi ya kuabudu katika maisha na masuala mengine mengi.

"Ni mkutano mkubwa sana ambao pia washiriki watapata kujua shughuli ambazo jumuiya yetu imefanya kwa jamii kwa kipindi cha miaka 85 tangu kuanzishwa kwake hapa nchini mwaka 1934," amesema Chaudhry.

 

 

Alisema mbali ya kuchangia katika sekta ya elimu kwa kujenga na kumiliki, pia wamesaidia mikoa mbalimbali huduma za maji kwa kujenga visima vya kutoa huduma hiyo bure.

“Tumeweza kujenga misikiti kuanzia ngazi ya vijiji, wilaya, mikoa na miji mikubwa na vilevile kushiriki kutoa misaada katika majanga ambayo yametokea Tanzania kupitia shirika letu la Humanity First," amesema.

Amesema washiriki wote watalala eneo la mkutano ambalo lina mahema na huduma zote za kijamii.