Mahakama yataifisha V8 iliyosafirisha wahamiaji haramu

Gari lililokamatwa likisafirisha wahamiaji haramu ambalo limetaifishwa na kuwa mali ya Serikali. Picha na Mary Sanyiwa

Muktasari:

  • Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Iringa, imeliitaifisha gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 iliyotumiwa kuwasafirisha wahamiaji haramu 16.

Mufindi. Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, imelitaifisha  gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 iliyotumika kuwasafisha wahamiaji haramu 16 na kuwa mali ya Serikali, baada ya washtakiwa hao kukiri kosa hilo.

Pia imewahukumu washtakiwa hao 16, raia wa Ethiopia adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja kwa kosa la kuingia nchini bila kibali. Washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini hiyo, hivyo wamepelekwa gerezani.

Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa April 12, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Benedict Nkomola baada ya kuwatia hatiani kwa kosa hilo, baada ya kukiri kutenda kosa hilo.

Waethiopia hao walitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa Idara ya Uhamiaji, Aprili 6, 2024 wakati wanapita Tanzania, huku wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T803 CVW, aina ya Toyota Land Cruiser V8.

Walipopandishwa kizimbani mahakamani hapo, upande wa mashtaka uliomba ahirisho kutokana na kutokuwa na mkalimani kwa ajili ya kuwatafsiria washtakiwa hao waliposomewa mashtaka yao.

Leo walipopandishwa tena kizimbani baada ya kupatikana mkalimani, wamesomewa shtaka la kuingia nchini bila kibali na mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali, Balius Namkambe.

Wahamiaji haramu wakitoka katika ukumbi wa Mahakama  baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja. Picha na Mary Sanyiwa

Baada ya kusomewa shtaka hilo na kuulizwa iwapo ni kweli, washtakiwa wote wamekiri kutenda kosa hilo, ndipo Mahakama ikawatia hatiani na kuwahukumu adhabu hiyo.

“Kutokana na kukiri kwenu kutenda kosa, Mahakama hii imewatia hatiani kwa kosa la kuingia nchini bila kibali kama mlivyoshtakiwa na Jamhuri, Mahakama inawahukumu adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kifungo cha miaka mitatu jela, mkishindwa kulipa faini hiyo,” amesema Hakimu Nkomola na kuongeza:

“Pia, Mahakama inatoa amri ya kutaifishwa kwa gari walilokuwa wakisafiria washtakiwa na kuwa mali ya Serikali.”

Kabla ya Mahakama kutoa adhabu hiyo, mwendesha mashtaka, wakili Namkambe aliiomba Mahakama iwape adhabu kali kwa mujibu wa sheria na akaiomba Mahakama hiyo iamuru gari walilokuwa walilitumia kuwasafiria itaifishwe kuwa mali ya Serikali.

Kwa mujibu wa wakili Namkambe, gari hilo lilikutwa limetelekezwa katika msitu wa Sao Hill na dereva aliyekuwa akiwaendesha alitoroka baada ya kubaini kuwa anafuatiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, wakili Namkambe ameishukuru Mahakama hiyo kwa kutoa adhabu hiyo kwa mujibu wa sheria.

 “Hii iwe fundisho kwa watu wengine kwa sababu mwenye gari, sisi tunatambua kuwa ndio mhalifu,” amesema Wakili Namkambe na kuongeza:

“kwa kuwa ametoroka, tunaendelea kumtafuta, endapo tukimpata atashtakiwa kwa kosa lake, kama atakuwa Mtanzania atashtakiwa kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu, lakini bado tunaendelea kumtafuta.”

Wakili Namkambe amesema kuwa gari hiyo ni ya tatu kukamatwa ikiwa na wahamiaji haramu kati ya Machi na Aprili, mwaka huu.

“Kibaya zaidi ambacho kinatuudhi ni kitendo cha kutumia namba za Serikali. Hivyo, kwa sasa tutakuwa wakali zaidi kwa sababu wanazubaisha askari wetu wa usalama barabara wasiweze kuwasimamisha. Hili ni jambo baya sana, lakini tunaendea kulikemea kwa nguvu zote,” amesisitiza Namkambe.

Pia, Wakiki Namkambe amewaonya wananchi ambao wanatumia mianya hiyo kutumia mali zao kusafirisha wahamiaji haramu kuacha mara moja kwa sababu idara ya uhamiaji imeweka utaratibu mzuri kwa wahamiaji kupitia katika ofisi hizo kwa ajili ya kuhakiki hati zao za kusafiri kisha kuendelea na safari zao.