Majaji: Hakuna uthibitisho kuwa Club House 'imepigwa pini' na Serikali

Muktasari:

  • Kutokana na kutokuwepo kwa uthibitisho wa Club House kuzuiwa hapa Tanzania, majaji wa Mahakama Kuu wamesema Mahakama haiwezi kutamka kuwa mdai ana haki ya kutumia Club House ikisema hakuna mawasiliano yasiyo na mazuio, lakini lazima yawe ni kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam iliyosikiliza shauri la kikatiba dhidi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema hakuna uthibitisho kuwa Serikali ndio iliyozuia kupatikana kwa mtandao wa Club House.

Mtandao huo uliojipatia umaarufu mkubwa nchini ukitumika katika mijadala mbalimbali ikiwamo ya kisiasa na matukio mazito, ulianza kutopatikana nchini Agosti 2023 na kumekuwa na hisia kwamba ni Serikali ya Tanzania kupitia TCRA ndio imezuia upatikanaji wake.

Mtandao huo kwa sasa hupatikana tu pale ambapo mtumiaji amepakua programu ya Virtual Private Networks (VPN), programu ambazo nyingi ni za kulipia, sio za bure na kwa sheria za Tanzania, mtumiaji atalazimika kusajili VPN anayoitumia.

Hata hivyo, jopo la majaji watatu, Fredrick Manyanda, Dk Ubena Agatho na Dk Angelo Rumisha katika hukumu yao waliyoitoa Mei 3, 2024, wamesema mikataba ya kimataifa imetoa haki ya upatikanaji wa habari, lakini haki hiyo ina mipaka kwa mujibu wa sheria.

Madai ya ukiukwaji Katiba

Katika kesi hiyo namba 27860 ya mwaka 2024, mdai Paul Kisabo, alimshitaki Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekinolojia ya Habari kama mdaiwa wa kwanza, TCRA kama mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania (AG) kama mdaiwa namba tatu.

Kisabo ambaye katika shauri hilo alijitambulisha kama mtumiaji mzuri wa mtandao wa Club House, alieleza kuwa kuzuiwa kutumia Club House kunakiuka Katiba ya nchi ya mwaka 1977 na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Haki alizodai zimekiukwa ni pamoja na haki ya uhuru wa mawazo na kujieleza, kutafuta, kupata na kusambaza habari, kujumuika na raia wengine wa Tanzania katika mijadala, na pia kuwa na haki mbalimbali kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa.

Katika madai yake, Kisabo alieleza kuwa TCRA imeweka vikwazo katika kutumia Club House na kwamba njia pekee ya kufikia mtandao huo ni kupitia VPN ambayo humwezesha mtumiaji kuingia katika tovuti ambazo maudhui yake sio ya umma.

Kulingana na Kisabo, Club House ni mtandao wenye umuhimu mkubwa katika mawasiliano ya kila siku kwa kuwa inaruhusu mijadala ya moja kwa moja na inaruhusu mtu kuweza kusikiliza majadiliano au mazungumzo yaliyorekodiwa.

Serikali kwa upande wake, kulingana na hukumu hiyo, ilikanusha kufanya jambo lolote baya na kukanusha pia kuzuia upatikanaji wa Club House hapa nchini na kusisitiza kuwa haimiliki mtandao huo, hivyo hawawezi kusema kama umezuiwa ama la.

Hiki ndicho walichokisema majaji

Katika hukumu yao kwenye hoja ya kuzuia upatikanaji wa Club House, majaji walisema mdai alisema mdaiwa namba mbili ambaye ni TCRA ndiye mwenye dhamana ya usimamizi wa mitandao, ndiye anayehusika kufanya Club House isipatikane Tanzania.

Mdai aliegemea kwenye ripoti ya OONI inayosema kuwa kuanzia Agosti 13, 2023, TCRA imezuia upatikanaji wa Club House lakini majaji wakasema baada ya kuipitia na kubaini ripoti hiyo sio hitimisho kwa kuwa inazungumzia kushuku kuwa Club House imezuiwa.

OONI ambalo ni shirika lisilo la Kiserikali (NGO) lenye makao yake makuu Roma, Italia lilifanya majaribio ya upatikanaji wa Club House nchini Tanzania kati ya Mei 1,2023 hadi Novemba 23, 2023, ambao wenyewe walisema hakuna uthibitisho wa uzuiaji huo.

Hata hivyo, majaji katika hukumu yao walisema ripoti hiyo ya OONI ni ya kutiliwa mashaka kwa sababu mbalimbali kwa vile mdai hakuwasilisha ushahidi kutoka OONI wala hapakuwepo kiapo kutoka shirika hilo, ambaye ndiye mwandishi wa ripoti hiyo.

Majaji walisema mwandaaji wa ripoti hiyo alipaswa kuiwasilisha kortini kama kielelezo, au shahidi ambaye anaiwasilisha kama kielelezo ni lazima aieleze mahakama namna alivyoipata nyaraka hiyo na kwa kufanya hivyo angeisaidia Mahakama kuipima.

Wakirejea majibu ya wadaiwa ambao ni taasisi hizo tatu za Serikali, majaji hao walinukuu wakisema TCRA haijazuia upatikanaji wa Club House na kueleza zaidi kuwa ni mtengenezaji mwenyewe wa Club House anaweza kutoa ufafanuzi wa upatikanaji wake.

TCRA ilisisitiza wao sio watengenezaji wa mtandao huo, hivyo hawana uwezo wa kuzuia upatikanaji wake na kwamba mamlaka hiyo kwa kutumia wataalamu wake wabobezi wanaweza kuzuia maudhui, lakini hilo ni lazima lifanyike kwa mujibu wa sheria.

Katika hukumu yao, majaji hao walisema ripoti ya OONI imeshindwa kuishawishi Mahakama kwamba mdaiwa wa pili (TCRA), alizuia upatikanaji wa Club House hapa Tanzania na mleta madai ameshindwa kubeba dhamana ya kuthibitisha hilo.

“Tulitarajia mdai angekuwa na ushahidi ambao ungeonyesha ni kwa namna gani uzuiaji wa Club House unavyofanyika.

“Ripoti ya OONI iliyoambatanishwa na kiapo cha mdai iko wazi kwamba inabashiri Tanzania imeanza kuzuia Club House. Ripoti ya OONI haijathibitisha madai hayo ya kuzuiwa. Kukosekana kwa uthibitisho huo, madai yanabaki kuwa uvumi,” walisema.

Hivyo, katika hukumu yao, majaji hao walikubaliana na mdai kuwa anayo haki ya kikatiba na kulingana na mikataba ya kimataifa kutumia Club House bila vikwazo visivyo vya kisheria, na kusisitiza kuwa hakuna haki wala uhuru ambao hauna mipaka.

Kutokana na kutokuwepo kwa uthibitisho wa Club House kuzuiwa hapa Tanzania, Mahakama haiwezi kutamka kuwa mdai ana haki ya kutumia Club House ikisema hakuna mawasiliano yasiyo na mazuio, lakini lazima yawe ni kwa mujibu wa sheria.