Majaliwa atoa maagizo kuhusu kikokotoo, usimamizi hifadhini

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utunishi wa Umma, George Simbachawene na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega bungeni jijini Dodoma, leo Aprili 15, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Muktasari:

  • Serikali imesema itafanya tathmini ya kanuni mpya ya kikokotoo kwa kuzingatia sheria za kazi.

Dodoma. Serikali imesema imesikia kilio cha kanuni mpya ya kikokotoo na kwamba itaendelea kufanya tathmini kwa kuzingatia sheria za kazi.

 Pia, Serikali imewataka wasimamizi wa hifadhi za Taifa kuzingatia sheria wanaposhughulika na wanaodaiwa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 15, 2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifanya majumuisho kuhusiana na hoja zilizotolewa na wabunge walipokuwa wakijadili hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge iliyopitishwa. Kesho ni zamu ya bajeti ya Tamisemi.

Licha ya wabunge kutoa hoja mbalimbali, hata hivyo hoja tano za wabunge ndio zilikuwa zikisubiri majibu ya Waziri Mkuu wakati wa majumuisho.

Hoja hizo tano zilizotolewa na wabunge zaidi ya mmoja ni kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo, mawaziri kutoa ahadi hewa, tozo ya laini za simu ya Sh2,000 na Sh10,000 kuchangia bima ya afya, katikakatika ya umeme na mauaji ya watu kwenye hifadhi ikiwamo wananchi kuvamiwa na wanyama kama tembo, mamba na nyani.


Kuhusu kikokotoo

Majaliwa amesema hoja hiyo imelenga kuitaka Serikali kufanya maboresho ya ulipaji wa mafao ya wafanyakazi kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii na kwamba Serikali iongeze wigo wa utoaji wa elimu ya kanuni mpya za mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga ulewa wa pamoja.

“Hoja hii kwa mujibu wa kanuni mpya ya ulipaji wa mafao ulioanza kutumika Julai Mosi, 2022 kwa kuzingatia tathmini ya uhimilivu na uendelevu wa mfuko iliyofanyika katika kipindi husika.

“Serikali imesikia, ushauri, maoni na kupokea maoni mbalimbali kupitia wadau wakiwamo waheshimiwa wabunge, wafanyakazi na vyama vya waajiri na wafanyakazi wenyewe.

“Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wafanyakazi wanaostaafu na itaendelea kufanya tathmini ya kuzingatia sheria za kazi, ili kufikia hatua nzuri ambayo haitazua malalamiko mengi,” amesema.

Majaliwa pia amesema kuhusu utoaji elimu kuhusu kanuni za mafao kwa watumishi, Serikali itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa jamii ikiwemo mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali.

“Nitumie fursa hii kumtaka Waziri wa Kazi na Ajira wasimamie kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa wa kutosha pamoja na mjadala ambao wanaendelea nao juu ya kikokotoo ambacho kimekuwa kinashauri na makundi ya wadau mbalimbali,” amesema.


Hoja ya uhalibifu wa wanyama

Pia, Majaliwa amejibu hoja ya uharibifu unaofanywa na wanyama pori iliyotolewa na mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko, kwamba Serikali inafahamu baadhi ya changamoto za wanyama pori kuvamia makazi, mashamba na kusababisha madhara kwa wananchi waishio karibu na hifadhi.

“Madhara hayo ni pamoja na ulemavu, vifo na uhalibifu wa mali. Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kukabiliana na wanyama waharibifu, uanzishaji wa vituo vya ulinzi kwa maofisa wanyama pori,” amesema.

Ameongeza:“Kwa upande mwingine kumekuwa changamoto ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro baina yao na askari hali ambayo pia imekuwa ikisababisha majeruhi kwa wananchi na askari wa hifadhi.”

“Nitumie fursa hii kuwakumbusha wasimamizi wa hifadhi kuzingatia taratibu wakati wa kushughulikia changamoto za uvamizi hifadhini. Kwa upande mwingine niwasihi wananchi kuheshimu pia mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuacha tabia ya kuingia hifadhini kiholela, kuingiza mifugo, kufanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi na uwindaji haramu,” amesema Majaliwa


Mawaziri kutotekeleza ahadi

Majaliwa pia amejibu hoja ya mbunge wa Sumve, Masalali Mageni aliyelalamika kuhusu mawaziri kutotekeleza hadi.

Akijibu hoja hiyo, Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 na ahadi za viongozi katika maeneo mbali mbali kupitia mipango ya bajeti ya kila mwaka.

Utekelezaji unafanyika unaendelea mpaka mwezi Juni mwaka huu 2024/2025 ambao ndio mwaka wa fedha.

Kwa hiyo ahadi zote ambazo zimetolewa tunatarajia pia kuzitekeleza katika kipindi hiki kwa zaidi ya asilimia 90.


Tozo ya laini za simu

Kuhusu hoja ya mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby ya kutaka kuongeza tozo ya Sh2,000 kwa kila laini ya simu, amesema sheria ya bima ya afya kwa wote ya mwaka 2023 imeanzisha mfuko kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na kubainisha vyanzo vya fedha vya mfuko huo.

“Serikali itaendelea kupokea mapendekezo ya uendeshaji wa mfuko ikiwemo vyanzo vya mapato na kufanya maboresho kadiri inavyofaa,” amesema.

Walichosema wabunge

Mfano, hoja ya kikokotoo ilitolewa na wabunge Ester Bulaya (Viti Maalum), Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Kasalali Mageni (Sumve) na Florent Kyombo (Nkenge) ambao wote wameitaka Serikali kukaa na wafanyakazi na kuirejesha sheria hiyo bungeni.

Mbunge wa Viti Maalumu anayetokana na vyama vya Wafanyakazi, Jane Jerry yeye amesema yawezekana elimu ya kikokotoo haijatolewa ipasavyo kuainisha faida na hasara kwa kuwa wafanyakazi wako gizani, hawaelewi wanacholipwa kimetokana na nini na kwamba elimu inahitajika.

Kinachopingwa na wafanyakazi ni kanuni mpya ya kikokotoo ya mafao ya mkupuko kuwa asilimia 35 badala ya asilimia 50 kama ilivyokuwa awali.

 “Kuteleza si kuanguka, turudi tukae, tuwasikilize, hizi ni pesa zao Serikali inaweka, wapeni mafao kwa mkupuko kwa asilimia 50, hiyo nyingine muwape kidogo kidogo.

“Yale mafao ya mkupuo ndiyo yanayowasaidia, si hiki ambacho mnawapa kila mwezi, wakiweka misingi haya mengine yatakuwa ya kawaida,” amesema Bulaya.

Naye Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni akichangia kuhusu kikokotoo amesema inawezekanaje mfanyakazi mwenye uzoefu wa kushika fedha na maisha akistaafu Serikali iamue kumtumzia fedha zake.

Kwa upande wake Gambo ametoa mifano ya jiinsi wastaafu wanavyopunjwa na kanuni mpya ya kikokotoo kwamba;

“Kwa yule ambaye mshahara wake kwenye kiwango cha wakurugenzi, labda milioni 3.720 (Sh3 milioni) kwa kikokotoo cha kabla ya Julai 2014 angepata milioni 266 (Sh266 milioni) kwa kikokotoo cha sasa angepata milioni 133 (Sh133 milioni) ambayo tofauti yake anakuwa amepunjwa milioni 135 (Sh135 milioni).”