Majaliwa: Komesheni ukiritimba Tanesco

Muktasari:

  • Majaliwa amesema Wizara ya Nishati iendelee kusimamia kupunguza au kuondoa kabisa mrundikano wa maombi ya kuunganisha huduma za umeme

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukomesha ukiritimba na ucheleweshaji wa huduma za kuunganishiwa umeme.

Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 19, 2024 wakati akifunga maonyesho ya wiki ya nishati iliyokuwa ikifanyika katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.

“Wizara ya Nishati iendelee kusimamia kupunguza au kuondoa kabisa mrundikano wa maombi ya kuunganisha huduma za umeme,” amesema.

Majaliwa amelitaka Tanesco kuhakikisha ukiritimba na ucheleweshaji wa huduma hiyo unakomeshwa.

Amesema anatambua kuwa wapo baadhi ya wapima (surveyors) ambao hufanya ucheleweshaji wa makusudi kwa wateja.

Amesema vitendo hivyo havikubaliki kwani vinakinzana na dhamira ya Rais Samia Sukuhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wote wameunganishwa na huduma ya umeme.

Pia amewataka wakala, mikoa na ofisi za kanda ziweke utaratibu wa kukutana na kutatua kero zao.

Amesema watendaji mnayo majibu ya changamoto za wananchi nendeni kwenye maeneo yao na kushughulikia kero zilizopo kama mlivyofanya kwa wabunge.

Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imewekeza katika miradi ya sekta ya nishati zaidi ya Sh8.18 trilioni kwa muda wa miaka mitatu. 

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema sekta ya nishati ni mtambuka kwa sababu inalisha sekta nyingine nyingi, hivyo ikitikisika inatikisa na maeneo mengine pia.

Lakini amesema maendeleo makubwa ambayo wanayashuhudia katika awamu ya sita, yote yanategemea nishati.

Amesema bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) limeleta mambo mazuri, kwanza umeme lakini pia wingi wa maji yaliyopo pale unaashiria kuwa hawatasikia tena tatizo la maji katika mikoa ya karibu.

Amesema wanatarajia kuwa Serikali itaweka miundombinu ya kutunza maji hayo ili yatumike kwenye usambazaji wa mikoa ya jirani.

“Lakini ukiacha hilo, hili tumeshalisema bungeni na sasa nalisema tuanzishe gridi ya maji kama vile tulivyokuwa na gridi ya umeme. Hapendezi kipindi cha mvua kuna maji mengi lakini yanapotea,” amesema.

Amesema lazima wajipange na maendeleo yao na kwamba sasa wanaendelea kukamilisha ujenzi wa bwawa la JNHPP, hivyo maji yatakuwa mengi sasa ambayo yatakuwa yakipita baada ya kukamilisha kazi ni lazima kutafuta namna ya kuyazuia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk David Mathayo amesema suala la uwajibikaji kwa jamii katika maeneo ambayo yana uwekezaji wa miradi ya gesi limekuwa halitekelezwi kikamilifu.

“Jamii katika maeneo yenye uwekezaji wa gesi hazinufaiki kwa rasilimali inayovunwa katika maeneo yao. Si jambo la ajabu kufika katika kijiji kimegubikwa na umasikini huku wawekezaji wakivuna gesi kwa wingi,” amesema.

Amesema ni rai ya kamati hiyo kuwa Serikali iangalie jambo hilo ili raslimali za gesi asilia zinufaishe wananchi na wasione kama vile ni laana kwa rasilimali hiyo kuwa katika maeneo yao.

Awali, Mhandisi Mkuu Mipango ya Uendeshaji wa Gridi ya Taifa wa Tanesco, Zubeda Chuma amesema hivi sasa kuna wakati wanazima mitambo kutokana na mahitaji ya umeme nchini kuwa  madogo kulingana na uzalishaji.

“Hivi sasa (saa 9.00 alasiri) tumezima mitambo mitano kwa sababu umeme ni mwingi kuliko mahitaji. Na sasa tuna ziada ya Megawati 175 za umeme,” amesema.

Amesema lakini ziada hiyo ambayo inatokana na umeme kuanza kuzalishwa katika mradi wa JNHPP, inatofautiana kutokana na hali ya mahitaji nchini.

Mradi wa uzalishaji wa umeme wa JNHPP wenye thamani ya Sh6.6 trilioni, utazalisha Megawati  2,115.