Makalla anavyojitofautisha na Makonda

Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaendelea na ziara yake katika mikoa sita ya Nyanda za Juu Kusini ambapo hadi sasa wametembelea mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya  huku akitarajiwa kumalizia mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Katika ziara hiyo inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amekuja na mtindo tofauti wa kufanya kazi ambao unamtofautisha na mtangulizi wake.

Katika ziara hiyo, Makalla amekuja na mtindo tofauti wa kusikiliza kero za wananchi ambao ni tofauti na Makonda, aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi jukwaani ambao mtu mmoja mmoja hupewa kipaza sauti na kueleza kero yake.

Makalla ameanzisha utaratibu mwingine wa “kusikiliza kero kisayansi” kwa kukaa pamoja na watendaji katika halmashauri husika na kuanza kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na watendaji husika kupewa jukumu la kuhakikisha wanazitatua.

Mtindo huo wa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi unazingatia suala la faragha zao ili kulinda heshima ya anayetoa changamoto na anayelalamikiwa, jambo linaloweza kuongeza chuki katika jamii.

Usikilizaji wa kero hizo unaongozwa na Makalla, ambaye anakuwa na timu ya watendaji na wataalamu wa halmashauri wanaokuwa pembeni yake kwa ajili ya kutoa majibu na mrejesho kwa wanaowasilisha kero hizo.

Hata hivyo, katika mchakato huo, Makalla amekuwa akisisitiza kuwa hawatazigusa wala kuziingilia kero za wananchi zilizopo mahamakani kwa sababu chama hicho kinaheshimu utawala wa sheria. Wanawapatia wananchi ushauri wa kukata rufaa pale inapobainika wameshindwa kesi.

“Mambo yaliyoko mahakamani yanamalizwa huko huko na mhimili huo, tutakachowasaidia ni yale mashauri yanayohitaji mambo ya utawala, yasiyoingilia Mahakama, ukija kwenye mkutano wa hadhara usilete suala lililopo mahakamani.

“Tutakuwa tunawadanganya watu kwamba hili lipo mahakamani tutakusaidia, si kweli, lazima wakati mwingine tuwe wakweli, tunafuata utaratibu,” alisema Makalla katika moja ya mikutano yake uliofanyika Katavi.

Mtindo huo mpya ulitangazwa na Makalla Aprili 13 mkoani Katavi, akisema utakuwa endelevu ili kulinda uhuru wa mtu anayetoa kero dhidi ya taasisi na viongozi wa Serikali, huku akisisitiza kwamba mbinu hiyo ni njema, haizui tafrani wala kelele kwa wananchi.

Hatua hiyo ilipigiliwa msumari na bosi wake, Dk Nchimbi aliyesema hivi sasa chama hicho kinasikiliza kero na malalamiko ya wananchi kwa njia bora aliyoiita ya kisayansi, huku akisisitiza hawasikiliza masuala yaliyopo mahakamani.

“Nitumie nafasi hii kumuunga mkono mwenezi wetu wa Taifa katika mambo tutakayoyashughulikia kama kero, hatuyagusi yaliyoko mahakamani, ndio utaratibu wa utawala bora. Moja ya sera ya CCM ni kusimamia utawala wa sheria.

“Wakati wote wajibu wetu utakuwa kuzihamasisha Mahakama zetu zitende haki bila kuziingilia katika uamuzi wake, nchi inayotaka kufanikiwa lazima isimamie utawala bora, ukijenga utaratibu wa kuingilia Mahakama siku moja utawaumiza,” alisema Dk Nchimbi, ambaye ni pia mwanadiplomasia.

Katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe ambayo wamefanya mikutano ya hadhara na kusikiliza kero kwa mbinu hiyo, Makalla amesema kumekuwa na mafanikio makubwa, ikiwamo kutatua changamoto zao kwa hali ya utulivu na staha.

Anasema akiwa kiongozi wa jopo hilo la kusikiliza kero, wanajivunia kuonana na wananchi wanaowasilisha changamoto zao na zinapatiwa ufumbuzi papo hapo, huku nyingine wakizibeba kwa ajili ya kuongeza msukumo katika utekelezaji wake.

“Asilimia kubwa ya kero nilizosikiliza zinatatulika na mkoa husika, hivyo zinazohitaji msukumo, tunazibeba kwa ajili ya kuongeza nguvu ili wananchi wapate majibu sahihi, lakini hata zilizotatuliwa tutakuwa tunafuatilia kwa karibu kuona utekelezaji wake,” anasema Makalla, aliyewahi kuwa mkuu wa mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Katavi na Kilimanjaro.

Wakati Makonda akiwa mwenezi wa CCM, alikuwa anawapa uhuru wananchi kuwahoji hadharani baadhi ya watendaji wa Serikali kuhusu changamoto ya jambo fulani au linalokwamisha huduma za msingi za kijamii.

Hata hivyo, zile kero zilizoonekana kuhitaji ufafanuzi zaidi, Makonda alilazimika kuwapigia simu mawaziri wa sekta husika ili kupata majibu au ufafanuzi unaojitosheleza.

Hatua hiyo ilifurahiwa na wananchi, lakini iliwapa wakati mgumu na hofu baadhi ya wananchi waliotoa kero zao na watendaji wa Serikali waliokuwa wakishindwa kutoa majibu sahihi na kufanya Makonda kuingilia kati kwa kuwabananisha.


Wasemavyo makada CCM

Baadhi ya makada wa CCM waliozungumza na Mwananchi wanasema hatua ya CCM kutumia mtindo huo mpya wa faragha ni jambo jema, inasaidia kumlinda anayetoa taarifa au madai dhidi ya taasisi au viongozi wa Serikali kuhusu changamoto au kero fulani.

“Ni jambo zuri, nawapongeza viongozi wetu kwa kuwa kusikiliza kero kwa faragha kunasaidia kuondoa chuki dhidi ya mtendaji wa Serikali unayemtuhumu, lakini inasaidia kutoa dukuduku lako kwa uhuru zaidi pasipo kuwa na hofu,” anasema Zakaria Mbukwa, mkazi wa Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mkazi mwingine wa mkoa huo, Andrew Ngindo anakubaliana na Mbukwa akisema njia wanayoitumia viongozi hao katika kusikiliza kero ndiyo bora kwa sasa na inalinda heshima ya anayetoa changamoto na anayelalamikiwa.

“Kusikiliza kero hadharani kunadhalilisha au kunasababisha mtendaji aonekane hatoshi katika nafasi yake kwa kushindwa kujibu kwa ufasaha changamoto za wananchi na inasababisha hofu.

“Kwa staili hii tupo katika mstari sahihi wa kusikiliza kero za Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyetu,” anasema Ngindo.

Naye Gerald Kikwembe anasema jambo hilo lipo sahihi kwa sababu litalinda utu na ubinadamu kwa anayetakiwa kusikiliza na mlalamikaji, huku akiunga mkono hatua ya CCM kutojihusisha na masuala yaliyopo mahakamani.

Hata hivyo, kada mwenzao Conard Sepetu alikuwa na maoni tofauti kuhusu jambo hilo akitaka kero zisikilizwe hadharani ili majibu yapatikane, kila mtu asikie. Anasema zikisikilizwa faragha zinaficha maovu ya wahusika.