Makonda: Walitaka kuniua kwa drone wakashindwa

Muktasari:

  • Asema kutokana na mapambano ya dawa za kulevya aliwindwa ili auawe.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewataka polisi mkoani humo kupambana na dawa za kulevya, akisema alinusurika kifo akipambana na dawa hizo alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema kutokana na mapambano hayo, aliwindwa na watu waliotaka kumuua, lakini wakashindwa.

Makonda alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Machi 2016 hadi mwaka 2020 alipoacha kazi na kwenda kugombea ubunge Kigamboni, lakini alishindwa kwenye mchakato wa kura ya maoni ndani ya CCM.

Akizungumza leo Aprili 20, 2024 na maofisa wa Polisi mkoani humo kupitia video iliyosambaa mitandaoni, Makonda amewataka kuwa na kauli moja dhidi ya dawa za kulevya, ili kufanya janga hilo kuwa historia.

Makonda Afungka vita vikali vya madawa ya kulevya,aliyokutana nayo Dar es salaam

“Nafahamu, nimekaa pale Dar es Salaam, haikuwa rahisi sana, mpaka sasa wauza dawa wakimwona Makonda wanaelewa, wamejaribu mbinu zote za kuniloga imeshindikana, wamejaribu mbinu za sumu imeshindikana, wamejaribu mbinu za kuniua imeshindikana,” amesema.

“Kuna kipindi ilikuwa inakuja drone (ndege isiyo na rubani) nyumbani kwangu na Jeshi la Wananchi limenisaidia, ningeshapotezwa. Wana teknolojia ya kukupiga hata kwa drone, lakini kwa mkono wa Mwenyezi Mungu ilishindikana,” amesema.

Amesema kutokana na hali hiyo kwa sasa anaishi kwa muujiza na kwamba, hata ujasiri alionao unatoka mbinguni.

“Ndiyo maana mnasema huu ujasiri wake unatoka wapi? Najua it’s from above (kutoka juu), yaani hapa haitokei, si kwa mzizi, hakuna junjalee hapa hakuna. It’s from heaven. Kama Mungu akiamua kuniachilia ni sekunde tu kwa sababu niko kwenye ‘tageti’ zao saa 24, siku saba,” amesema.

Amesema anajivunia vita hivyo, kwa kuwa anaamini alisaidia kuokoa watoto wa watu wasiangamie kwa dawa hizo.


Alivyotangaza watuhumiwa

Februari 3, 2017, akiwa Mkuu wa Moa wa Dar es Salaam, Makonda alitangaza majina 12 ya watu aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya.

Kama hiyo haitoshi, Februari 8, 2017 Makonda alitaja majina mengine 65 ya watuhumiwa hao, wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara maarufu, viongozi wa dini, wasanii na aliwataka waripoti kituo kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Ilipofika Februari 13, 2017 Makonda alikabidhi majina 97 ya aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga.

Licha ya juhudi hizo, hakuna aliyekamatwa akihusishwa na tuhuma hizo, hali iliyoelezwa na baadhi ya wachambuzi kuwa hatua hiyo ililenga kuwachafua.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipiga marufuku viongozi kutaja majina hadharani ya watuhumiwa wa dawa za kulevya.


Onyo wala rushwa

Katika hatua nyingine, RC Makonda amewaonya polisi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, akisema watapata laana na vizazi vyao.

“Mafanikio yoyote yale ya rushwa ni mbegu ya laana kwenye kizazi chako. Yaani unachukua rushwa kutoka kwa mwananchi wa kawaida, mnyonge, masikini, anajikuta anauza shamba, anafunga duka lake, pikipiki yake inaondoka, pesa zote unazopata kwa njia hiyo, ni laana ambayo watoto wako watavuna,” amesema. 

Amesema madhara yake pia ni kupata magonjwa: “Pesa utakuwa nazo, lakini wewe kazi yako ni kujitibu tu, sasa kwa nini uishi hayo maisha? Kuna watu huko mtaani hawana pesa, hawana cheo kikubwa utamkuta kwenye kijiwe cha kahawa ana amani sana, kwa sababu dhuluma haiko sehemu ya maisha yake.”

“Ndiyo maana nawasihi sana viongozi wa dini ni muhimu kuwafundisha watu madhara ya pesa ya rushwa, asikutishe mtu unaona anaendesha gari zuri, yawezekana hana hata amani, asikutishe mtu anaishi jumba zuri kuna watu wengine wana majumba mazuri, lakini hawana amani humo ndani,” amesema.

Akizungumzia usalama kwa ujumla, Makonda amewataka polisi kuungana na wadau wengine katika kukabiliana na uhalifu, ili kufikia ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kumfanya hata mgeni anapokuja anaondoka na habari njema akitangaza uzuri na uimara wa Jeshi la Polisi, utulivu na usalama wetu, amani ambayo ni nguvu kubwa inayowafanya Watanzania inakuwa sehemu ya kimbilio,” amesema.

Amesema mkutano huo ulilenga kujua matatizo ya jeshi hilo ili ajue jinsi ya kuwasaidia katika utendaji kazi na kuufanya mkoa huo kuwa bora.

“Bahati nzuri nimefanya kazi na Jeshi la Polisi kwa muda na upendo wangu kwenu sidhani kama unatiliwa shaka, kwa sababu najua huwezi kumnyooshea mtu kidole kama hujamwezesha, ukamtuhumu na kumlaumu wakati mazingira yake ya kazi hata huyajui,” amesema.

“Kwa hiyo nilitamani niyajue mazingira yenu ya kazi na mimi nikiwa mwenyekiti wa kamati ya usalama, nione nina mchango gani wa kuyafanya mazingira yenu yawe bora zaidi,” amesema.