Mambo matatu yatajwa sababu za kuongezeka watalii

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Daniel Masolwa akizungumza na waandishi wa habari Dodoma.

Muktasari:

  • Idadi ya watalii kuanzia Januari hadi Agosti 2023 imeongezeka kufikia watalii 1,131,286 kutoka watalii 900,104 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Dodoma. Vivutio vya wanyamapori, fukwe za bahari na kupanda Mlima Kilimanjaro ni vivutio vinavyotajwa kuchangia ongezeko la idadi ya watalii nchini.

 Katika kipindi cha Januari hadi Agosti, 2023 idadi ya watalii nchini imeongezeka kufikia watalii 1,131,286 ikilinganishwa na idadi ya watalii 900,182 walioingia kipindi kama hicho mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 25.7.

Aidha watalii walioingia nchini katika kipindi cha Agosti pekee wameongezeka kufikia 186,030 ikilinganishwa na watalii 158,049 walioingia nchini mwezi Agosti, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 9, 2023 Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk Daniel Masolwa amesema kati ya watalii walioingia nchini mwaka huu, watalii 236,047 waliingia kupitia Zanzibar sawa na asilimia 31.1 ya watalii wote.

“Aidha katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2023, pia tulipokea watalii kutoka Afrika ambapo idadi kubwa ilitoka Kenya watalii 128,753, Burundi 69,505, Zambia 38,398 na Rwanda 37,269,” amesema Masolwa.

Aidha idadi hiyo kwa watalii walioingia nchini kuanzia Januari 2023 ilikuwa ni watalii 146,877, Februari 144,019, machi 118,186, Aprili 96,852, Mei 106,497, Juni 146, 896, Julai 185,929 na Agosti walikuwa watalii 186,030.