Maofisa elimu wapewa miezi minane wanafunzi wajue Kiingereza

Muktasari:

  • Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Maksio Maganga amesema mitalaa ya elimu iendane na kasi ya ufundishaji, ili kuhakikisha watoto kuanzia elimu ya darasa la kwanza hadi la tatu wanajengewa uwezo  kufikia malengo ya kuinua kiwango cha elimu nchini.

Mbeya. Maofisa elimu ngazi ya mkoa na halmashauri wamepewa miezi minane kuhakikisha wanafunzi wa darasa la tatu katika shule za msingi nchini wanajua lugha ya kiingereza sambamba na kuwachukulia hatua walimu wasiotekeleza majukumu yao.

Pia, wameagiza wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la pili kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) ifikapo Desemba 2024.

Agizo hilo limetolewa leo Jumanne Aprili 16, 2024 na Mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Maksio Maganga wakati akifungua mkutano mkuu wa 10 wa Umoja wa  Maofisa Elimu Ngazi ya Mikoa na Halmashauri (Redeoa) kutoka mikoa 26 nchini uliofanyika katika ukumbi wa Edeni jijini hapa.

Maganga amesema mitalaa ya elimu iendane na kasi ya ufundishaji, ili kuhakikisha watoto kuanzia elimu ya darasa la kwanza hadi la tatu wanajengewa uwezo kufikia malengo ya kuinua kiwango cha elimu nchini.

Pia, amesisitiza kwamba maofisa elimu wahakikishe wanakamilisha miradi yote ambayo haijatekelezea sambamba na usimamizi wa ufundishaji kwa walimu na kuwatia moyo wanaofanya vizuri, huku wasiotekeleza majukumu yao kuchukuliwa hatua.

Baadhi ya maofisa elimu wa  ngazi za mikoa na halmashauri kutoka mikoa 26  walioshiriki mkutano wa 10 wa mwaka wa kujadili masuala mbalimbali ya mitaala ya elimu. Picha na Hawa Mathias

Amesema lengo ni kufikia malengo ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 23 ya kulinda mitaala ya sekta ya elimu nchini kuanzia ngazi za halmashauri na mikoa.

Amesema katika kuboresha sekta ya elimu kwa kipindi cha 2020  mpaka 2024  Sh1.41  trilioni  zimetumika  kuboresha  miundombinu ya elimu kama  madarasa, mabweni, maabara, matundu ya vyoo, hali iliyopunguza adha kwa wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Wakati huohuo, amesema Sh960 milioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa mabweni tisa kwa wanafunzi kwenye shule ya elimu maalumu nchini.

Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa umoja huo, Charles Mwakalila amesema licha ya Waziri wa Elimu, Profesa, Adolf Mkenda kutoa magari katika kila halmashauri na kutoa maelekezo kwa walimu kupatiwa kwa ajili ya kutembelea miradi, agizo hilo halijatekelezwa na badala yake kutumika ndivyo sivyo.

“Baadhi ya viongozi wa halmashauri wamekuwa wakitumia magari hayo kwa malengo yasiyokusudiwa na Wizara ya Elimu kwa matakwa yao binafsi, licha ya agizo la waziri mwenye dhamana,” amesema.

Mwenyekiti wa umoja huo, Juma Kaponda amesema lengo la mkutano huo ni kufanya tathimini ya maboresho ya mitaala ya elimu, ili uweke mikakati ya pamoja kufikia malengo yenye ushindani.

Amesema mbinu nyingine ni tathimini ya usimamizi wa elimu nchini ambayo italeta matokeo mazuri katika sekta ya elimu nchini.

Rais wa CWT, Leah Ulaya akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa elimu mikoa na halmashauri nchini jijini Mbeya.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Leah Ulaya amesema Serikali imejitahidi kupandisha madaraja na kulipa madeni mengi kwa walimu, lakini bado tatizo lipo kwenye ajira za walimu.

Amesema tofauti na miaka ya nyuma walimu walikuwa wakimaliza vyuo na kupata ajira, lakini kwa sasa lazima waombe hali inayokwamisha ufanisi.

“Upungufu wa walimu ni mkubwa kwa shule za msingi hata sekondari na kusababisha waliopo kuwa na mzigo mkubwa wa masomo na kuondoa ufanisi,” amesema na kuongeza:

“Hata mfumo wa kuomba ajira hatuubezi, lakini Serikali izingatie umri, mtu akiomba aangaliwe kwa muda huo. Zamani mtu alikuwa akimaliza chuo anapata ajira, hali ambayo ilikuwa bora sana,” amesema Leah.

Kwa upande wake, kaimu katibu mkuu wa chama hicho, Joseph Misalaba amesema mabadiliko katika mitalaa inakwenda kuleta tija, huku akieleza kuwa CWT itaishauri Serikali na Wizara ya Elimu kuwapa mafunzo walimu, ili kuendana na mabadiliko hayo.

“Hii mitalaa inakwenda kutubadilisha katika ufundishaji na kuongeza uelewa kwa wanafunzi, CWT itajitahidi kushauri Serikali na wizara kuongeza mafunzo kwa walimu, ili kufikia malengo,” amesema Misalaba.