Maporomoko ya  tope Mbeya yazua balaa

Muktasari:

  • Mvua iliyonyesha leo Aprili 14 imesababisha nyumba 20, ng'ombe na mifugo mingine kufukiwa na tope kutoka Mlima Kawetele

Mbeya. Zaidi ya nyumba 20, shule, mifugo na mashamba vimeharibiwa na tope zito lililosababishwa na Mlima Kawetere uliopo Kata ya Itezi, Wilaya ya Mbeya kumeguka kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Mvua hiyo iliyonyesha leo Aprili 14, 2024 imesababisha makazi  kuzingirwa na tope,  mifugo kusombwa huku ikiharibu miundombinu ya barabara ikiwamo kufukiwa kwa Shule ya Msingi Generation.

Tazama Maporomoko ya tope zito Mbeya

Tukio hilo linalodaiwa kutokea alfajiri ya leo limesababisha ng'ombe wanne, mbwa na kuku na mifugo mingine kusombwa na maji huku mali nyingine zikifukiwa kwa tope hilo kutoka mlimani.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kuhusu tukio hilo, baadhi ya waathirika wa mafuriko hayo ya tope, wamesema hadi sasa hawajui sehemu ya kuelekea na matumaini yao ni kwa Serikali kuona inawasaidiaje.

Mkazi wa eneo hilo, Upendo Mwakasendo amesema licha ya nyumba yake kuharibika, haijasababisha majeruhi wala vifo zaidi ya makazi yao kubomoka na shughuli iliyopo ni kuhamisha vyombo kutafuta hifadhi kwa wasamalia.

Amesema pamoja na jitihada zinazoendelea kuokoa mali zilizobaki, wanategemea msaada wa Serikali kwa kuwa wapo wananchi ambao hawana ndugu na makazi yao yamesombwa.

“Kwa maana hiyo, huu mlima bado, unaona unemeguka, mvua inaendelea kunyesha, hatujui tunaenda wapi kutafuta wasamalia, imesomba kila kitu.

“Hapa tunaomba Serikali itusaidie chakula, malazi ili tuone watoto wetu tunawaweka wapi, shule ndiyo hiyo nayo imefunikwa na tope...tunaomba msaada,” amesema Upendo.

Kwa upande wake, Halima Seif amesema katika mafuriko hayo amepoteza mifugo yake yote lakini familia yake iko salama kutokana na maeneo waliyokuwepo.

Amesema walianza kusikia kama kishindo cha wanyama kikigonga mlango, lakini walishtuka kusikia kila eneo la nyumba linasukumwa na maji kuingia ndani ndio wakaamka haraka.

“Kitu kikawa kinasukuma nyumba lakini ikasikika kama kelele nyingine nje, tukaamka haraka na kuona maji yanashuka mlimani kwa kasi na tope, tukatoka ndani.

“Mifugo yangu sikuifikiria zaidi ya watoto niliowashika haraka, tukatoka ndani, tukaona wananchi wengine wanahangaika, majirani wanaokoa vitu na sisi tukaanza kutoa baadhi ya mali,” amesema Halima.

Mkazi mwingine, Emanuel Esau amesema walikuwa wakijiandaa kwenda kanisani na kujikuta wakishindwa kutoka baada ya nyumba yao kuzingirwa na maji lakini walifanikiwa kutoka salama.

Amesema ng'ombe wake wanne waliokuwa nje, hajui kama wamefukiwa na tope au kuondoka na maji kwa kuwa usiku walikuwa salama pamoja na kuku kwenye banda, hajui walipo.

“Kwa jumla ni hasara kubwa kwa sababu ukiangalia hii nyumba nimeijenga kwa pesa nyingi kutokana na mazingira yake, hilo la mifugo sijui imefukiwa kwenye hili tope au wameenda na maji,” amesema Esau.

“Kwa sasa hatuna msimamo, tunarudi maisha mengine kujipanga, upya kusubiri hatima yetu japokuwa Serikali wamefika wameona hali halisi, tunasubiri kuona watatusaidiaje.”

Mmiliki wa Shule ya Generation, Baraka Nkoko amesema alipokea taarifa ya mafuriko alfajiri na kufika shuleni hapo na kuona miundombinu ikiwa imeharibika lakini walifanikiwa kuokoa nyaraka zote.

Amesema ni hasara kubwa iliyojitokeza na kwamba kwa sasa wanafikiria kufunga shule hiyo kwa muda ili kupisha ukarabati na hali kutulia.

“Kuna walimu walikuwepo hapa shuleni wakiandaa mitihani ya majaribio kwa darasa la nne, ndipo mmoja wao akanipigia, nikakuta hali ilivyo kama unavyoona, hasara ni kubwa.

“Mpango uliopo ni kuwataarifu wazazi na walezi wa wanafunzi kwamba tunafunga shule kwa muda wa wiki moja ili kuona hali itakavyokuwa, hili ni tukio la kwanza kutokea hapa Itezi,” amesema Nkoko.

Kauli ya serikali

Akizungumza baada ya kufika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanya tathimini kwa waathirika hasa wale wasio na malazi, wahakikishe wanapatiwa sehemu hizo wakati Serikali inaendelea kupambana kuhakikisha hali inakuwa sawa katika maeneo hayo.

Pia, ameagiza Kitengo cha Ardhi Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuacha kuwapimia wananchi viwanja eneo lenye changamoto hasa la mkondo wa maji, kwa kufanya hivyo, kutasababisha matatizo kama hayo ambayo yangeweza kuzuilika.

“Kwanza hakuna maafa kama inavyoelezwa mitandaoni, lakini naomba Halmashauri ya Jiji kufanya tathimini ya haraka kujua waliopata changamoto kuweza kuwapatia sehemu ya malazi.

“Lakini kitengo cha ardhi kuacha kuwapimia wananchi viwanja eneo lenye changamoto hasa maeneo yenye mkondo wa maji, vinginevyo ni kusababisha matatizo kama hayo,” amesema Homera.

Homera amelekeza pia shule zilizokumbwa na mafuriko hayo kutoendelea na masomo akieleza kuwa wanafunzi 250 waliokosa sehemu watapelekwa kwingine kwa usalama.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Malumbo Ngata amesema katika tukio hilo hakuna majeruhi wala vifo kwa binadamu licha ya maporomoko yaliyotokea na kuharibu makazi ya watu.

“Tulifika eneo la tukio mapema na kushuhuhudia maporomoko lakini tulijitahidi kufanya uokoaji, licha ya nyumba kufunikwa lakini hakukuwa na madhara kwa binadamu," amesema Ngata.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema wameandaa Shule ya Msingi Itezi kwa ajili ya kuwahifadhi waliopatwa na changamoto kuweka mizigo yao.

“Wakazi wa eneo hili la Itezi wameonesha ushirikiano na kuwajali wenzao, tunashukuru na tumeandaa eneo la Shule ya Msingi Itezi kwa ajili ya kuwaweka waathirika hawa,” amesema Malisa.