Mashimo ya viraka barabarani yawatesa madereva

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), uwekaji wa kiraka ni mbinu ya dharura inayofanywa kutoa mwanya kwa barabara iliyoathiriwa na mashimo iendelee kutumika.

Dar/Mikoani. Hivi unajua shimo la barabara linapochongwa ili kuwekwa kiraka linapaswa lidumu kwa saa 72 tu kabla ya kuzibwa?

Si hivyo tu, hata barabara inapokatwa kwa ajili ya kuwekwa kiraka, utekelezwaji wake unapaswa kufanyika kwa muda usiozidi saa 48.

Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), uwekaji wa kiraka ni mbinu ya dharura inayofanywa kutoa mwanya kwa barabara iliyoathiriwa na mashimo iendelee kutumika.

Licha ya matakwa hayo ya kitaalamu, watumiaji wa barabara nchini wanaeleza uhalisia tofauti, wakifafanua viraka vingi vinavyopaswa kuwekwa baada ya kukatwa au kuchongwa na mashine barabarani hudumu zaidi ya saa hizo.

Si viraka pekee, wanasema katika baadhi ya barabara, hasa zenye mashimo hukatwa kwa ajili ya kuwekwa viraka, lakini inachukua muda mrefu bila hilo kutekelezwa.

Hali hiyo kwa mujibu wa watumiaji hao, inasababisha ajali, msongamano na wakati mwingine huongeza gharama na usumbufu kwa watumiaji wa barabara kwa vyombo vyao kuharibika, lakini pia kusababisha ajali.

Hata hivyo, kuchelewa kwa ukarabati wa barabara baada ya kuchongwa ili kuwekwa kiraka, aghalabu husababishwa na mvua kama inavyofafanuliwa na Mkuu wa Idara ya Mipango wa Tanroads Dar es Salaam, Clever Akilimali.

Mazingira kama hayo, Machi 2015, eneo la Changalawe Mafinga, Mkoa wa Iringa yalisababisha ajali mbaya kati ya lori la mizigo la Kampuni ya Cipex na basi la Kampuni ya Majinjah Express lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam kugongana.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 42 na wengine 23 kujeruhiwa. Nyasio Pascal, aliyekuwa shuhuda wa ajali hiyo amesema aliliona lori hilo likijaribu kukwepa mashimo kwenye barabara hiyo ambayo ni nyembamba, mara likaanza kuyumba kulia na kushoto baada ya kukanyaga shimo, ndipo lilipofuata basi na kugongana nalo.


Uhalisia barabarani

Mwananchi imezungumza na watumiaji mbalimbali wa barabara, akiwamo Salum Abdallah, aliyekuwa akiendesha gari dogo kutoka Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam mwisho mwa wiki. Anasema baadhi ya mashimo barabarani yanapaswa kutengenezwa haraka ili kujinusuru na ajali.

“Kuna muda nilikwepa bonde lililochongwa, mbele kukawa na gari linakuja, ni Mungu tu alisaidia kuwahi kurudi kwenye mstari uelekeo, lakini ni changamoto sana,” anasema Abdallah.

“Kama mashimo yanachongwa ili kuwekwe viraka, basi yatengenezwe haraka, kuyaacha yalivyo ni hatari sana. Kuna ile ajali ilitokea Iringa miaka ya nyuma na kuua zaidi ya watu 40, chanzo ilikuwa mashimo. Kwa hiyo Serikali inapaswa kutengeneza barabara zake haraka,” anasema.

Lakini, Frank Edward aliyesafiri kwa gari dogo kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma hivi karibuni naye anaeleza uwepo wa mashimo na viraka vingi kwenye barabara. Anasema ukiachana na kuongeza muda wa safari, hali hiyo inahatarisha usalama kwa kuwa barabara hazijatulia, unaendesha unakwepa kwepa mashimo na nyakati za usiku hali inakuwa mbaya zaidi.

"Kuna wakati inabidi muanze kukwepa mashimo, unaona kabisa dereva anavyohangaika karibu atoke barabarani, ni hatari sana," anasema Edward.

Katika Mkoa wa Arusha nako, Amina Bakari anasema mashimo ndiyo changamoto kubwa katika barabara za eneo hilo, hivyo kuchelewesha watoto wanapokwenda shule.

Rukia William naye pamoja na mashimo na viraka, anasema kukosekana kwa vivuko ni changamoto nyingine katika barabara za Arusha. Katika maelezo yake alitolea mfano Barabara ya Serengeti iliyoharibika na kusababisha baadhi ya biashara zifungwe na kuathiri mapato ya Serikali.

Vyombo vya usafiri vya watumiaji wa barabara ya Kenyatta mkoani Mwanza, vinaharibika mara kwa mara kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, barabara ina viraka vingi.

Dereva wa daladala, Dickson Mwitta anasema barabara zenye mashimo yaliyokatwa ili kuwekwa viraka zinaharibu magari kwa asilimia 100.

“Lami inapokuwa hivyo (viraka) husababisha dereva kutumia muda mwingi awapo safari, maana hutembea kwa tahadhari kubwa ili kulinda chombo chake kisipate madhara na kulinda watumiaji wengine pia. Barabara za mjini kuwa mbovu kwanza ni taswira mbovu ya halmashauri yetu,” anasema Mwitta.

Dereva bodaboda, Fikiri Thobias anashauri kuliko Serikali kuweka taa za barabarani hata sehemu zisizo za lazima, ni bora zingefumua barabara zenye viraka, kuleta ahueni kwa watumiaji.

Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, mwenyekiti wa bajaji wilayani humo, Moses Miyo anasema ubovu wa barabara unasababisha kuharibika mara kwa mara kwa vyombo vyao vya usafiri.

"Changamoto ya ubovu wa miundombinu ni kubwa kwa sababu barabara ikiwa mbovu hatuwezi kupata faida, hata mmiliki baada ya kupata faida anapata hasara, kwa kuwa muda mwingi unakuwa unatengeneza vyombo hivyo," anasema Miyo.


Madereva wa mabasi

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi (Uwamata), Majura Kafumu anasema mbali na kuendesha kwa tahadhari kama wasafirishaji wa abiria, pia aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kuweka alama za hatari pindi wanapoona eneo la barabara si salama.

Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa, wakati mwingine uharibifu katika barabara huweza kutokea ndani ya muda mfupi tangu dereva kutua njia hiyo, hivyo ni muhimu ushirikiano wa karibu ukatolewa na wananchi.

“Ikiwa wananchi wana shaka na eneo fulani, basi waweke alama ili kuonyesha usalama ukoje katika eneo husika kuwasaidia madereva, wakati mwingine sisi tunaendesha ila hatujui hali halisi ikoje huko chini, unaweza kuona ni ufa mdogo, kumbe ni hatari,” anasema Kafumu.

Wakati yeye akisema hayo, mmoja wa wamiliki wa daladala jijini Dar es Salaam, Ghalib Mohammed anasema ubovu wa miundombinu ya barabara umekuwa ukisababisha kuharibika kwa magari, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji.

Wakati yeye akisema hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Salum Pazzy anasema wakiwa wasimamizi wamekuwa wakihakikisha wanaratibu usalama ardhini.

“Kama kuna shida ya miundombinu tunawaita wadau na kuwaambia, hivyo tumekuwa tunaratibu kwa namna hiyo kwa sababu suala la ujenzi liko chini ya Wizara ya Ujenzi,” anasema.

Ukongwe wa barabara tatizo

Umri wa barabara ni moja ya sababu inayofanya mamlaka zilazimike kuweka viraka vingi, kama inavyoelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Victor Seif.

“Umri unaweza kuwa umefikia lakini rasilimali za kufanya maboresho zinakuwa hazitoshi,” anasema Seif.

Katika ufafanuzi wake, anasema kitaalamu baada ya barabara kukatwa, kiraka kinapaswa kuwekwa ndani ya saa 48.

Lakini utekelezaji wa hilo, anasema unakwamishwa na changamoto ya upatikanaji wa lami kwa wakati kwa ajili ya kuziba mashimo.

“Kwa sasa tumepiga marufuku, wanapokata barabara wahakikishe inazibwa kwa wakati na tumekuwa tukifuatilia hili,” anasema Seif.

Anasema barabara nyingi ni mbaya zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma, zinatakiwa kufanyiwa matengenezo.

Hoja ya ukongwe wa barabara inazungumzwa pia na Meneja wa Tanroads mkoani Mwanza, Pascal Ambrose anayesema baadhi ya miundombinu hiyo ina muda mrefu.

“Mfano barabara ya kwenda Shinyanga na Musoma kutokea Mwanza ni za muda mrefu, kwa hiyo matabaka yake ya chini yamechoka, sasa maji yakiingia yanafumua na kusababisha viraka kuwa vingi, hali inayosababisha kuathiri usafirishaji, ikiwa ni pamoja na vyombo vya moto kuharibika,” anasema.

Pia, anasema viraka huwekwa kuondoa changamoto kubwa inayokuwepo, hata hivyo ni vigumu palipowekwa kiraka kufanana na pasipowekwa.

Kuhusu barabara ya Kenyatta, Ambrose anasema wana mpango wa kuifumua na kuijenga upya kwa njia nne na tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika, kinachosubiriwa ni fedha kutoka serikalini.