Matinyi aeleze mradi Bonde la mto Msimbazi utakavyotekelezwa

Muktasari:

  • Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema nyumba na majengo yote yanayopaswa kubomolewa katika eneo la Bonde la Mto Msimbazi yameshawekewa alama na wahusika wanafahamika na wanafahamu.

Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) itazingatia makubaliano yake na wakazi wa eneo la Bonde la Mto Msimbazi, jijini Dar es Salaam wakati wa ubomoaji wa nyumba zao.

 Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi utakaoigharimu Serikali Sh675 bilioni, lengo lake ni  kupunguza athari za mafuriko, kuongeza matumizi bora ya ardhi, kuzia mmomonyoko wa udongo, kurejesha uoto wa asili na kuruhusu maji kwenda baharini.

Ufanikishaji wa hayo ni kupitia ujenzi miundombinu ya kukabiliana na mafuriko, karakana ya mabasi yaendayo haraka eneo la Ubungo maziwa, kupanua Mto Msimbazi, ujenzi wa daraja la Jangwani, bustani ya jiji na uendelezaji wa maeneo ya makazi na biashara na uondoaji wa taka ngumu.

Matinyi ameeleza hayo leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa mradi huo, hali ya mafuriko na mvua nchini  na maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano.

Kiongozi huyo amesema mradi huo utaanza rasmi Aprili 15, ukisimamiwa na Tarura na nyumba zilizopo Jangwani na kandokando ya Mto Msimbazi zitaondolewa.

Matinyi amesema nyumba na majengo yote yanayopaswa kubomolewa katika eneo lile yalishawekewa alama na wahusika wanafahamika na wanafahamu.

“Wakati Tarura ikipanga mambo yote haya ya ubomoaji itaanza  mradi huu wa ubomoaji  kwa kuzingatia makubaliano yake  na wakazi wa eneo  hilo na utaanza rasmi Jumatatu Aprili 15,2024. Utaanza kwa kubomoa nyumba  eneo la Jangwani Kando na Mto Msimbazi,” amesema.

Kuhusu hatua ya kuwaondosha wananchi, Matinyi amebainisha kuwa baada ya tathmini kufanyika na wahusika kulipwa fidia walipaswa ndani ya miezi sita wawe wamekamilisha taratibu za kuondoka, ili kazi ianze.

Hadi kufikia Februari 26, 2024, Matinyi amesema Tarura ilikuwa imelipa fidia ya Sh52.61 bilioni kwenye akaunti za wamiliki wa nyumba 2,155 kati ya 2,329 ambao waliandikishwa kwenye daftari la kwanza.

Ameongeza kuwa Tarura sasa inakamilisha taratibu za malipo ya fidia kwa wahusika 446 waliopo kwenye daftari la pili ambao hawakufanyiwa tathmini kutokana na sababu mbalimbali.

“Tarura itashirikiana na ofisi za Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam ikizingatiwa Bonde la Msimbazi linapita zaidi ya hamshauri moja,” amesema.

Matinyi ameeleza kuwa mradi huo utakamilika mwaka 2028 na utagharimu Dola milioni 260 za Marekani (Sh675 bilioni). Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).