Matumizi holela ya antibaotiki tishio nchini, Ummy afanya mabadiliko

New Content Item (2)

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Kutokana na ongezeko la matumizi holela ya dawa za antibaotiki, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameondoa jukumu la usimamizi wa maduka ya dawa kutoka Baraza la Famasi na kupeleka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameliondolea jukumu la usimamizi wa maduka ya dawa Baraza la Famasi nchini na kuipa mamlaka hayo rasmi Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA)

Maamuzi hayo yametokana na ongezeko la matumizi holela ya dawa za antibaotiki ambalo kwa sasa limekua tishio nchini kwa kuongeza usugu wa vimelea dhidi ya dawa mwilini ‘Antimicrobial resistance AMR’.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 9, 2023 katika ukurasa wake wa wa mtandao wa kijamii wa X wakati akijibu hoja ya Frank Arabi aliyehoji kuhusu matumizi sahihi ya dawa za antibaotiki.

“Usugu wa vimelea dhidi ya dawa mwilini ni tishio kubwa la afya kwa jamii ya Watanzania, hivyo Serikali imeweka mikakati madhubuti ili kukabiliana na tatizo hilo kwa kuimarisha udhibiti.


“Tumeondoa usimamizi wa maduka ya dawa kutoka Baraza la Famasi na kupeleka majukumu haya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),” amesema.

Waziri Ummy amesema kumekuwepo na matumizi yasiyo sahihi ya dawa nchini na hivyo kufanya dawa nyingi za antibiotiki kuwa na ufanisi mdogo katika kutibu magonjwa.

“Pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa za antibiotiki, tatizo hili kwa kiasi kikubwa linachochewa na  baadhi ya wataalam wetu kwenda kinyume na kanuni na miongozo ya taaluma,” amesema Waziri Ummy.

Pamoja na hayo amewataka wahudumu wa afya hasa madaktari na wafamasia kusimamia jukumu hilo ili Watanzania wapate uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa.

Takwimu zinaonyesha matumizi ya dawa dhidi ya vimelea nchini yanakadiriwa kufikia asilimia 62.3, sambamba na makadirio ya usugu kwa asilimia 59.8 huku utafiti ukionyesha wengi hutumia antibaotiki bila ushauri wa daktari.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Moshi ulionyesha asilimia 92.3 ya wauzaji 82 walisambaza dawa hizo bila cheti cha dakktari mwaka 2017.

“Utafiti wa mwaka 2021 zaidi ulionyesha kati ya watumiaji watumiaji 960 jijini Dar es salaam, asilimia 70.6 walijibu kwamba waliacha kutumia antibiotiki baada ya dozi kukamilika, na asilimia 42.3 hutumia iwapo zilibaki nyumbani au kwenda kununua ikiwa ndugu au rafiki zilimsaidia,” amesema Profesa kutoka Idara ya Viuavijasumu Muhas, Mecky Isaac Matee.

Amesema asilimia 57 kati ya wanafunzi 374 wa vyuo vikuu viwili vya Moshi walinunua wenyewe dawa bila ushauri wa daktari kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2021.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah amesema lazima kuwe na usimamizi wa sheria kwa dawa zinazoathirika na usugu wa vimelea.

Amesema hiyo itasaidia ziweze kujilikana na kufuatiliwa kwani hata kwa sasa idadi ya antibaotiki ngapi zinaingia nchini na zinatoka kwa cheti hilo jawabu haliwezi kupatikana.

“Usimamizi wa sheria, dawa hizi ambazo tunaziita zinaathirika na usugu wa vimelea ni dawa za cheti, tuhakikishe dawa hizi zinapatikana kwa cheti tu hivyo tutadhibiti usugu, wafamasia wasimamiwe vizuri kwa kufuatiliwa kwa hakika ili kuziuza kwa kuzingatia sheria,” amesema Hezekiah.