Matumizi ya rada yaokoa wachimbaji migodini

Muktasari:

Teknolojia ya rada hiyo hupiga picha za satelaiti kwenye eneo la uchimbaji na kutoa taarifa kwa mtaalamu iwapo kuna dalili za ukuta au mwamba kuanguka. Hivyo kusaidia kuokoa majanga yanayoweza kuepukika.

Arusha. Katika kuelimisha wananchi na washiriki wa maonyesho ya usalama na afya mahali pa kazi Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeleta vifaa mbalimbali ili kutoa fursa kwa washiriki hao kujifunza teknolojia za kisasa za uokoaji.

Hayo yamebainishwa leo Jumamosi, Aprili 27, 2024 na Meneja Usalama kutoka GGML, Isack Senya wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho hayo yanayofanyika kwenye viwanja vya General Tyre jijini Arusha na kuratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (Osha).

“Kama kawaida GGML kwa kutambua umuhimu wa afya na usalama kazini na ikiwa ni tunu yetu ya kwanza, GGML ina wawakilishi zaidi ya 45 kwenye maonyesho haya wanaotoa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya afya na usalama kazini,” amesema Senya.

Senya amesema katika maonyesho hayo wamekwenda na vifaa mbalimbali ikiwamo rada maalumu, ambayo ina uwezo wa kutambua ukuta wenye  udhaifu au unaoweza kuanguka pindi shughuli za uchimbaji mgodini zikiendelea.

Amesema rada hiyo hutoa ripoti mapema ili kuondoa watu kwenye maeneo husika iwapo ukuta au mwamba huo unataka kuanguka.

“Kifaa hiki kinaangalia eneo la uchimbaji na kinavyozunguka kinapiga picha za satelaiti. Picha hizi zinarejeshwa kwenye mfumo na kuona kama kuna mwenendo wowote wa ukuta unaoweza kuleta athari, inamtahadharisha mtaalamu na kuchukua hatua stahiki.

“Rada hii ilisaidia sana mwaka 2007 ambapo kulitokea maporomoko makubwa ya ukuta lakini kutokana na kifaa hiki, yalibainika mapema na kuchukua hatua stahiki ikiwamo kudhibitiwa,” amesema.

Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Dk Kiva Mvungi amesema wamekwenda katika maonyesho hayo wakiwa na mambo mengi zaidi na tofauti kulingana na kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “mabadiliko ya tabianchi na athari usalama na mazingira.”

“Tumeona madhara mbalimbali yaliyotokana na mabadiliko ya tabianchi hivyo tumeona ni muhimu sasa kuhakikisha elimu tunazotoa zinajikita kwenye maeneo hayo,” amesema na kuongeza pia katika banda hilo wanatoa huduma za awali za afya ikiwamo upimaji wa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu.

Mbali na rada pia amesema GGML wameleta boti ya uokoaji majini, vifaa vya uokoaji katika uchimbaji chini ya ardhi pamoja na kutoa elimu kuhusu majanga makubwa na vidhibiti majanga ambayo yanaweza kuepukwa.

Amesema katika maonyesho hayo tayari wameshatoa mafunzo ya namna ya kujikinga na kukabiliana na majanga ya moto kwa akina mamalishe 50 wa mkoani Arusha pamoja na kuwagawia mitungi ya gesi ya kupikia.

Pia amesema wanatarajia kutoa mafunzo kwa madereva pikipiki kuwaelimisha namna ya kuzingatia usalama pindi wawapo katika shughuli zao.

Amesema kutokana na mifumo imara ya udhibiti majanga pamoja na kuzingatia masuala ya afya na usalama kazini kwa muda wa zaidi ya miaka 14 sasa ndani ya GGML, hakuna kifo kilichotokea kutokaa na shughuli hizo za uchimbaji.