Mawasiliano yarejea barabara ya Moshi – Arusha

Baadhi ya magari yakipita katika Daraja la Mto Sanya mpakani mwa kata za Kia na Bomang'ombe, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro baada ya mawasiliano ya barabara yalikatika kurejea

Muktasari:

 Mamia ya wasafiri waliokuwa wakisafiri ndani na nje ya Kilimanjaro kwenda maeneo mbalimbali nchini walishindwa kuendelea na safari zao kutokana na kutopitika kwa barabara hiyo

Hai.  Mawasiliano katika barabara kuu ya Moshi-Arusha yameanza kurejea baada kuondolewa kwa magogo na miti iliyokuwa imeziba Daraja la Sanya lililopo katika eneo la Kwa Msomali, wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na mafuriko.

Kuanzia saa saba usiku wa kuamkia leo Aprili 14, 2024, mamia ya wasafiri waliokuwa wakisafiri ndani na nje ya Kilimanjaro kwenda maeneo mbalimbali nchini walishindwa kuendelea na safari zao kutokana na kutopitika kwa barabara hiyo kulikosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Hata hivyo, hali hiyo ilisababisha adha kwa watumiaji wa Barabara Kuu ya Moshi – Arusha na kusababisha msongamano wa magari yaliyokuwa yamebeba abiria na yale ya binafsi yaliyokuwa yanakwenda sehemu mbalimbali nchini.

Akizungumzia kurejea kwa mawasiliano katika barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Kilimanjaro, Motta Kyando amesema barabara ilianza kupitika baada ya kuondolewa kwa magogo yaliyoshushwa na mafuriko ya mvua kuziba barabara katika Daraja la Mto Sanya.

“Tumetoa magogo na magari yameanza kupita, magari yalianza kupita kwenye muda ya saa moja asubuhi na yanapita upande mmoja baada ya tuta la upande mwingine wa barabara kumeguka, tayari mkandarasi ameanza kazi,” amesema.

 “Hili ni Daraja la Sanya linalopokea maji kutoka Sanya Juu, nimeona watu wengi wakiongea kwenye mitandao daraja limejengwa juzi tu, sio hilo, ni daraja jingine la  Mto Biriri ambalo limekuwa likipokea maji kutoka Longido na mengine Sanya Juu na tangu tumejenga hili daraja, hapajawahi kutokea changamoto yoyote.”

Akizungumzia adha ya kukatika kwa mawasiliano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa amesema hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokeza zaidi ya watu kupoteza muda kwa waliokuwa wakisafiri kwenda mikoa mbalimbali hapa nchini.

“Maji yalileta magogo na miti na wakati huo daraja lilikuwa limejaa maji kutokana na mvua zinazonyesha maeneo mbalimbali, lakini baada ya kuyaondoa, barabara sasa inapitika, hadi sasa hakuna madhara yoyote ya kibinadamu isipokuwa kusimama kwa safari,” amesema Mkalipa.