Mbinu mpya uendeshaji Kikoba kidijitali

New Content Item (1)

Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TCB) Adam Mihayo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Toboa na Kikoba.

Muktasari:

  • Benki ya TCB yaja na kampeni kuwezesha vikundi kufanya kazi kidijitali

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo Tanzania (TCB) imezindua huduma ya Kikoba Mix Kidijitali kuwezesha wanachama kutengeneza kikundi mtandaoni na kuwa na uwezo wa kuweka michango, bila kujali mtandao wa simu wanaotumia.

Mkurugenzi wa TCB, Adam Mihayo ameeleza hayo leo Mei 9, 2024 alipozindua kampeni ya ‘Toboa na Kikoba’ itakayowezesha vikundi kufanya kazi kidijitali.

Aina mbili za vikoba zimezinduliwa, cha kwanza kikihusisha watumiaji wa mitandao ya simu ya Tigo, Halotel, Airtel na Vodacom, na cha pili kikihusisha watumiaji wa mitandao tofauti kikipewa jina la Kikoba Mix.

Mihayo amesema kuanzishwa Kikoba Mix kunaondoa changamoto ya awali iliyowakabili baadhi ya wanakikundi wasiokuwa na namba ya simu ya mtandao husika ambayo kikundi kimetengenezewa.

Amesema wanachana waliweza kujiunga lakini walishindwa kuchangia michango moja kwa moja kutokana na mfumo kutowaruhusu.

“Uzinduzi wa Kikoba hiki unakuja katika wakati ambao watu wanatamani kuwa na uwezo wa kuamua namna na wakati wa kufanya miamala yao, njia hii ni salama kwa uwazi na inawezesha kufanya miamala kwa haraka,” amesema Mihayo.

Amesema uendeshaji wa Kikoba Mix na kile cha kawaida unasimamiwa na TCB chini ya miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hivyo kinaendeshwa kwa kufuata misingi iliyowekwa na Serikali.

“Niwatie imani kuwa wateja wetu wote waliojiunga kupitia vikundi hivi, fedha zao zitakuwa salama. Hili limeanzia hapa lakini litaenda nchi nzima ili Watanzania waelewe kampeni ya Toboa na Kikoba ni nini, namna ya kujiunga na kikundi na imekuja na utaratibu mzuri wa kuwawezesha kila mtu,” amesema Mihayo.

Sonia Tuteka, Katibu wa Kikoba cha Good Hope amesema awali matumizi ya laini tofauti yalikuwa kikwazo kufikia huduma za Kikoba kidijitali tofauti na sasa kila mwanachama bila kujali mtandao aliopo anaweza kufikia huduma hizo.

“Tulikuwa tukikusanya fedha tunakubaliana tufanye kitu lakini tunashindwa kupata muafaka kwa sababu huyu ana laini hii, mwingine ile inakuwa changamoto tofauti na sasa,” amesema Sonia.

Anelisya Mwakamelo, Mwenyekiti wa Bodaboda Millenium Tower II amesema kwa sasa bodaboda zaidi ya 20 wamejiunga katika kikoba hicho.