Mbunge adai Tanroads ilimpa kazi mkandarasi asiye na vifaa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Kwenye jimbo hilo ekari 5,000 za mashamba zimesombwa na mafuriko na hivyo kuwepo tishio la njaa.

​​​​​​Morogoro. Mbunge wa Ulanga (CCM), Salim Hasham ameutupia lawama Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Morogoro kwa kumpa kazi mkandarasi asiye na vifaa, jambo ambalo limesababisha kuchelewa kwa ujenzi wa barabara na kuchochea kupanda kwa bei za vyakula.

Amedai mkandarasi huyo alipewa mradi wa kujenga barabara inayounganisha Ulanga na Ifakara, hata hivyo, amedai tangu alipopewa mradi huo, hajafanya kazi yake kutokana na kutokuwa na vifaa.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 29, 2024 mbunge huyo amesema kutokana na changamoto ya barabara nyingi kutopitika, nauli zimepanda na hata bei za vyakula hazishikiki kwa kuwa magari hayawezi kwenda kubeba mizigo mikubwa katika jimbo hilo.

“Mvua zimeleta athari kubwa kwa upande wa barabara na imesababisha kwa umbali wa kilometa 68, ambao nauli yake iliyokuwa Sh10, 000, kupanda hadi Sh50,000.

Pia magari yanayopeleka bidhaa Ulanga hayafiki na hata yale ya abiria hayafiki kabisa baada ya barabara ya Ulanga – Ifakara kuhribika, amesema.

“Hali hiyo imesababisha kupanda kwa bidhaa katika jimbo hili, kwa mfano chumvi iliyokuwa ikiuzwa Sh300 – hadi Sh500 kwa kilo, sasa inauzwa Sh1, 500 – 2,000. Sukari iliyokuwa Sh3, 000 sasa Sh7, 000 kwa kilo moja. Unga uliokuwa Sh1, 200 kwa sasa unauzwa Sh3, 200 hili linasababishwa na changamoto ya barabara ambayo inaendelea katika jimbo letu,” amesema.

Mbunge huyo amesema jimbo hilo linapitia wakati mgumu kwa kukosa barabara kwa zaidi ya miezi minne sasa, lakini licha ya kutoa taarifa kwa Tanroads, hakuna kinachofanyika.

“Binafsi nimejaribu kuwasiliana na Meneja wa Tanroads mkoa wa Morogoro kumweleza adha ambayo tunaipitia katika jimbo letu, akanijibu kwamba mvua zinanyesha na hawezi kutengeneza Barabara.

“Wakati huohuo baada ya hali kuwa mbaya, nilitoa vifaa vyangu nikatengeneza baadhi ya maeneo kwa ajili ya wananchi wangu na hali ikatengamaa. Inaonekana hawa Tanroads hawajui majukumu yao.

“Hakutakuwa na mawasiliano kati ya Ulanga na Mahenge, tumewaambia Tanroads zaidi ya mwezi mzima wachepushe ile barabara ili ikitokea imekatika basi wananchi waendelee kupita hata kwa pikipiki, hawajafanya chochote,”  amesema.

 Ameongeza kuwa barabara ya Ulanga – Ifakara imeshapata mkandarasi lakini hafanyi kazi yoyote.

“Hili kwetu ni jambo la ajabu na tunamuomba ajitafakari, kwa maana wananchi wanapata changamoto ya barabara hizo kutotengenezwa kwa wakati kumbe wakandarasi wamepewa kazi huku wakiwa hawana vifaa,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Alinanuswe Kyamba amesema wako kazini kuhakikisha hali inatengamaa katika maeneo yote ambayo yana changamoto na wakandarasi wenye miradi husika wako saiti wakitekeleza majukumu yao.

“Ni kweli tangu Novemba 2023 mkoa wetu umepata mvua ambazo ziko juu ya wastani, na mvua hizi hazinyeshi Ulanga peke yake. Kama mlivyoona wilaya za Malinyi, Mlimba na Kilombero nazo zilikuwa katika hatari kubwa lakini pamoja na changamoto hizo sisi tuko kazini na hata wakandarasi wetu wako kazini kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” amesema.

Hata hivyo, meneja huyo amesema baada ya mvua kuwa nyingi walimzuia mkandarasi anayelalamikiwa kuwa angekwangua barabara ile ingeharibika tena na maeneo yasingepitika.

“Kuhusu mkandarasi kupewa kazi bila kuwa na vitendea kazi, hilo sio jukumu langu, siku hizi mkandarasi anapatikana kwenye mfumo na akishapatikana tunaingia makubaliano, anaanza kazi. Sisi tunachoangalia ni mradi ukamilike ili wananchi wautumie,” amesema Kyamba.

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jimboni humo, ekari 5,000 za mashamba zimesombwa, hivyo tani 500 za chakula ambazo walitarajia kuvuna zimeondoka na mafuriko.

Wakati Tanroads ikisema hayo, wananchi wa kata ya Ketaketa, Mbuga na Ilonga kutoka katika jimbo hilo, wameunga mkono kauli ya mbunge wao wakiiomba Serikali kuhakikisha barabara zinapitika ili kuokoa maisha ya wananchi wengi.

“Wananchi tulio wengi hapa Ulanga, mashamba yetu yamesombwa na maji na tunategemea chakula cha kununua. Watu wa Tanroads wawasimamie vizuri wakandarasi wanaowaweka, watujengee barabara ili zianze kutumika na vyakula kuletwa,” amesema Alfred Richard wakati akizungumza na Mwananchi.

Sarah Daniel amesema vyakula vimeadimika sababu ya barabara za kupitisha magari ya mizigo, hivyo iko haja kwa Serikali kuja na mpango wa muda mfupi wa kupatikana kwa barabara.