Mbunge azikataa ‘English Medium’ za Serikali

Mbunge wa viti maalumu (CCM) Taska Mbogo akizungumza wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25 leo Aprili 18, 2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

Mbunge Taska Mbogo ametamka bungeni kwamba manispaa na halmashauri kuanzisha shule za mkondo wa Kiingereza zinakwenda kinyume na sera ya elimu bila malipo na zinajenga mataba kwa Watanzania


Dodoma. Mbunge wa viti maalumu (CCM), Taska Mbogo amezichongea manispaa na halmashauri kwa kuanzisha shule za mkondo wa Kiingereza ‘English Medium’ na kulipia ada, hali ambayo ni tofauti sera ya Serikali ya elimu bila malipo.

Mbogo amesema hayo leo Alhamisi Aprili 18, 2024 wakati akichangia taarifa ya makadirio ya mapato na mtumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Manispaa na halmashauri nchini zimezua tabia ya kujenga shule zenye mkondo wa Kiingereza kwa maana ya ‘English Medium’. Bunge linapitisha Bajeti ya Tamisemi ambayo ndani yake kunakuwa na pesa ambayo inakwenda kuhudumia shule za msingi za Serikali nchini.

“Pia, Bunge linapopitisha bajeti hiyo ina maana linataka elimu bora kwa Watanzania wote, kwa watoto wote wa Kitanzania,” amesema Mbogo.

Mbogo amesema uanzishaji wa shule hizo zenye mkondo wa usomaji wa Kiingereza unawataka wananchi walipe ada kwa ajili ya watoto wao, na kwamba siyo wananchi wote wenye uwezo wa kulipa ada kwenye shule hizo.

“Je, Wizara ya Tamisemi inataka kuniambia kwamba Serikali sasa hivi inafanya biashara kwa kufungua shule zenye mkondo wa Kiingereza.

“Sababu shule hizo zinalipiwa na si wananchi wote wenye uwezo wa kulipia, kama kuna haja ya kufundisha Kiingereza ni kwa nini hiki Kiingereza kisifundishwe kwenye shule zote nchini.

“Lakini, zaidi ya hapo shule hizi zinatumia walimu ambao wanalipwa mshahara na Serikali, iweje walimu wale walipwe mshahara na Serikali halafu halmashauri au manispaa ziseme kwamba zimetengeneza kitega uchumi, wakati walimu wanaofundisha pale ni walimu ambao wanalipwa na Serikali,” amesema Mbogo.

Mbogo amesema shule zenye mkondo wa Kiingereza zinachukua walimu bora. “Mawazo yangu ni kwamba wale walimu bora wangetawanywa kwenye shule zote nchini waweze kuwafundisha wanafunzi wote.”

Amesema shule hizi zinakwenda kujenga matabaka nchini Tanzania.

“Hapa tulipo tutakwenda kujenga matabaka ya watoto wa walionacho na watoto wa wasiokuwa nacho. Na haya matabaka ina maana tutakuwa tumeyatengeneza sisi wenyewe, kama sera ya Serikali ni elimu bila malipo basi sioni sababu ya halmashauri au manispaa kujenga shule ambazo zinahitaji kulipa ada.

“Mwaka jana nilimuuliza waziri wa elimu atoe ufafanuzi, alisema shule hizo hata kama zimejengwa watoto watasoma bure. hayo yalikuwa ni majibu ya waziri wa elimu,” amsema bila kumtaja jina.

Ameshauri shule hizo zibinafsishwe kwa watu binafsi ili waweze kuziendesha kwa sababu Serikali huwa haifanyi biashara.

Shule za mkondo wa Kiingereza

Kata zote za Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, zimeelezwa zitakuwa na angalau shule moja ya awali na msingi inayofundisha kwa kutumia lugha ya Kiingereza.

Februari 26, 2024 timu ya wataalamu na madiwani kutoka Halmashauri ya Kwimba jijini Mwanza walikwenda Manispaa ya Kinondoni kujifunza namna ya uanzishaji na uendeshaji wa shule za msingi zinazotumia mchepuo wa lugha ya Kiingereza (English Medium).

Wataalamu na madiwani hao walitembelea Shule ya Msingi Oysterbay inayotumia mchepuo wa Kiingereza.

Pia, Mkoa wa Ruvuma ina mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza inayoitwa Chief Zulu Academy inayojengwa mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Manispaa ya Songea.

Mradi unatekelezwa kwa gharama ya Sh500 milioni kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, na wanafunzi wa mwanzo wameanza Januari 2024.

Sera ya elimu bila malipo ilianza rasmi nchini baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2015 chini ya Rais John Magufuli na imeendelea chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Alia shule za Mpanda Mjini wanafunzi kukaa sakafuni

Mbogo ameliambia Bunge kuwa,  shule kadhaa za msingi zilizopo Mpanda mjini mkoani Katavi, wanafunzi wengi wanakaa sakafuni, upungufu wa walimu na matundu ya vyoo kulingana na idadi ya wanafunzi.

Mbogo ambaye ni mbunge kutoka Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, amesema hayo kwa kujielekeza zaidi kwenye kero zilizopo katika shule za Mpanda mjini.

Hoja zake zimehusu taarifa ya makadirio ya mapato na mtumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25, ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyowasilishwa bungeni na waziri wake, Mohamed Mchengerwa.

“Kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Pale Mpanda mjini shule ni chakavu, nikianza na shule ya Shanwe iliyoanzishwa mwaka 1959 ina wanafunzi 1,959 na ina walimu 18, shule ina madarasa 11. Ina upungufu wa madawati 316, watoto kuanzia darasa la tatu na la nne wanakaa chini.

“Watoto wanaokaa kwenye madawati ni kuanzia la tano, la sita na la saba. Hii shule ya Shanwe inayopatikana Mpanda Mjini.

Amesema Shule ya Semula iliyoanzishwa mwaka 1974 ina wanafunzi 1,582, walimu 16 na madarasa nane huku ikiwa na upungufu wa madawati 568.

“Kuna shule ya Mingumila ina wanafunzi  3,082 lakini ina walimu 19 ambao ina upungufu wa madawati wa 500 ina maana watoto wanakaa chini, matundu ya vyoo 13 kwa wavulana na 13 kwa wasichana.

“Kuna shule nyingine ya Mpanda mjini, shule ya Msakila ina wanafunzi 2,370 ina upungufu wa vyoo, ina upungufu wa madawati na ina upungufu wa walimu. Kuna shule nyingine shule ya Nyerere pale Mpanda mjini.

Shule zote zinapatikana Mpanda mjini ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Katavi,” amesema Mbogo ambaye alishindwa kumalizia maelezo yake kutokana na muda wake wa kuchangia kumalizika.