Mbunge Sitta apaza sauti malipo ya mafao ya wastaafu

Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta akizungumza wakati akichangia makadirio ya mpato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25 leo Jumanne, Aprili 16 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Asema ana orodha ya walimu 53 wanaohenya kufuatilia mafao.

Dodoma. Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta amesema baadhi ya wastaafu wamelazimika kukopa fedha kupeleka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, ili walipwe mafao yao.

 Amesema hayo leo Jumanne Aprili 16, 2024 akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25.

Ametaka wanapowathamini wafanyakazi wa sekta ya afya na walimu wakati wakiwa kazini, wafanye vivyo hivyo wanapostaafu kwa sababu wamefanya kazi kubwa ya kuwaendeleza watu kiafya na kielimu.

“Kwa mfano mimi hapa mezani kwangu nina orodha ya walimu 53 ambao wamehenya wakitumikia shule za sekondari, msingi, Wizara ya Elimu sasa hivi wanahangaikia mafao yao,” amesema.

Amesema kuna haja ya Tamisemi kushirikiana na Hazina, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuona ni jinsi gani ya kuliweka sawa jambo hilo.

Sitta aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ametaka suala hilo lishughulikiwe, ili wastaafu wanapomaliza kazi na kwenda kutafuta mafao hasa katika Mfuko wa Hifadhi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wapate kwa wakati.

Amesema wastaafu wanapokwenda huambiwa kiasi cha fedha wanazostahili, lakini wanashindwa kupewa kwa sababu walipopandishwa madaraja mishahara yao haikurekebishwa.

“Najua juhudi zilizochukuliwa na Serikali za kuona wanaanza kurekebisha mshahara, lakini bado kuna tatizo hasa wale waliostaafu siku nyingi. Tunaomba hili lishughulikiwe, nina orodha ya walimu wanaolia machozi,” amesema.

Amesema baadhi yao wanaamua kwenda kukopa na kupeleka kwenye mifuko hiyo, ili wapewe mafao yao.

Sitta aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ametaka watu waliofanya kazi kwa uaminifu wasipitie kipindi hicho.

Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka ametoa angalizo kwa Tamisemi kuhusu Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) akimtaka waziri kuiangalia kwa sababu walimu hawako salama, hawana furaha, akieleza wamekuwa na manung’uniko mioyoni.

“Taasisi hiyo ipo jambo, hili haliwezi kuwa sawa. Walimu hawako salama na hii tume, hebu chungulia-chungulia huko,” amesema.