Mchengerwa afafanua matukio ya ubadhirifu yanayosambaa mtandaoni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amesema matukio ya ubadhirifu yanayosambaa mitandaoni ni ya mwaka 2017.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amesema taarifa nyingi juu ya matukio ya ubadhirifu wa fedha zinazoandikwa sasa katika mitandao ya kijamii yalitokea kati ya mwaka 2017 hadi mwaka 2021.

Kufuatia hilo Mchengerwa amesema watendaji wote ambao wamekuwa wakitajwa kushiriki katika ubadhirifu huo walichukuliwa hatua.

Ametoa kauli hiyo katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa mikoa walioteuliwa siku chache nyuma iliyofanyika Ikulu jijini hapa leo Jumatano Machi 13, 2024.

Mchengerwa amesema kufuatia taarifa za kuwapo kwa ubadhirifu huo, aliposhika nafasi ya Waziri wa Tamisemi waliwachukulia hatua za kinidhamu ikiwamo kuwasimamisha kazi.

“Wengi wao wako mahakamani na kesi zao zinaendelea, tumeshawaeleza watendaji wote kuwa hatutasita kuendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya watendaji wanaofanya kazi kwa mazoea na kukwamisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali ambazo Rais unadhamiria kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali,” amesema Mchengerwa.

Amesema kipindi hiki ndiyo ambacho Tamisemi imefanya kazi kubwa ya kushughulika na kero za wananchi huku akieleza kuwa watendaji wake wamekuwa wakifanya kazi kubwa.

Ili kuhakikisha kazi hizo zinafanyika kikamilifu, Tamisemi imekuwa ikihakikisha nidhamu inasimamiwa na pale zinapotokea changamoto hatua kali zilichukuliwa kwa watumishi wazembe, wala rushwa na wanaofanya kazi kwa mazoea.

Amesema anaamini kuwa wakuu wa mikoa waliopangwa katika ngazi mbalimbali watafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha dhamira ya Rais ya kufikisha huduma kwa wananchi inafanikiwa.