Mchengerwa katikati ya Mwalimu Nyerere, Mkapa

Muktasari:

  • Katika hotuba ya kurasa 136, ina nukuu tano za hayati Mwalimu Julius Nyerere na nukuu moja ya hayati Benjamin Mkapa alizozitumia kuelezea utendaji kazi wa Tamisemi.

Dodoma. “Ubadhirifu serikalini unarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.” Ni kauli ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitumia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa kukemea ubadhirifu serikalini.

 Nukuu hiyo imo katika hotuba ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1977, ikiwa ni miaka 10 baada ya Azimio la Arusha.

Mchengerwa amemnukuu Mwalimu Nyerere leo Jumanne Aprili 16, 2024, aliposoma hotuba ya wizara hiyo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25, yanayohusisha mafungu ya Tamisemi, Tume ya Utumishi wa Walimu na mikoa inayojumuisha halmashauri 184.

Ametumia nukuu hiyo kueleza Tamisemi imeendelea kuchukua hatua kwa watumishi wanaotekeleza majukumu yao kinyume cha sheria, taratibu na kanuni.

“Katika mwaka 2023/24 watumishi 225 wamechukuliwa hatua za kinidhamu, kati yao wakurugenzi ni 13, wakuu wa idara 30, watumishi wa sekta ya ujenzi 15, sekta ya afya wanane na 159 wa kada nyingine,” amesema.

Mchengerwa ametumia nukuu nyingine ya Mwalimu Nyerere: “Hakuna shida yoyote ya watu ambayo tunaweza sema kuwa haituhusu.”

Nukuu hii ilitolewa na Mwalimu Nyerere mwaka 1962. Mchengerwa ameitumia kuzungumzia namna Tamisemi inavyoshiriki utatuzi wa kero za wananchi katika mikoa na wilaya.

“Hayati Baba wa Taifa aliwahi kusema “Hakuna shida yoyote ya watu ambayo tunaweza sema kuwa haituhusu – J.K. Nyerere 1962 Dar es Salaam.”

Amesema Tamisemi inaendelea kuyaenzi maneno hayo, akieleza mwaka 2023/2024 wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya wameendelea kutekeleza shughuli mbalimbali, ikiwemo kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

“Hadi Machi, 2024 jumla ya kero 16,938 zimepokewa na zilisikilizwa katika ngazi ya mikoa na wilaya, jumla ya kero 7,322 zimetatuliwa na kero 9,616 zipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.”

“Kero hizo zilizopokewa na kusikilizwa zipo katika sekta mbalimbali zikiwemo za utawala, afya, elimu, ardhi, maji, barabara na nishati,” amesema.

Mchengerwa amesema Tamisemi ina Kituo cha Huduma kwa Wateja (Contact Centre) kwa lengo la kushughulikia malalamiko na kero za wananchi.

“Hadi Machi, 2024 kituo kimehudumia wananchi 23,896. Masuala mengi yaliyopokewa na kusikilizwa kutoka kwa wananchi yalikuwa katika sekta za afya, elimu na ardhi.”

“Kituo kimekuwa msaada kwa wananchi katika kupunguza na kutatua changamoto zinazowakabili kupata taarifa sahihi zinazohitajika, mathalani miongozo mbalimbali, ufafanuzi, hususanl wakati wa kuomba ajira pindi zinapotangazwa, ubadilishaji wa machaguo ya tahasusi, uhamisho wa watumishi katika mamlaka za serikali za mitaa, hivyo kuwapunguzia gharama za safari ya kuja Dodoma kushughulikia kero husika,” amesema.

Waziri huyo akizungumzia kuongezeka kwa mapato ya ndani, alieleza kunasadifu dhana ya hayati Mwalimu Nyerere, aliyekuwa na maono kuhusu ukusanyaji wa mapato akiamini yanapaswa kukusanywa kwa ufanisi, ili kuwezesha maendeleo endelevu na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa maneno yake, alielezea kuwa: “Mapato ni damu ya maendeleo. Bila ya mapato hakuna maendeleo. Nchi masikini siyo masikini kwa sababu hazina maliasili, zana, au watu hodari. Zipo nchi tajiri duniani ambazo hazina haya pia. Masikini ni masikini kwa sababu mapato yake ni madogo.”

Mchengerwa amesema kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato kumewezesha kuongezeka kwa matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo kutoka Sh194.80 bilioni zilizotumika hadi Machi, 2023 ikilinganishwa na Sh226.05 bilioni zilizotumika hadi Machi, 2024.

Kwa kutumia nukuu ya Mwalimu Nyerere: “Taifa husomesha watu wake kwa faida ya Taifa.”

Mchengerwa amesema: “Napenda kunukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoyasema mwaka 1966 kuhusu umuhimu wa Serikali kugharimia elimu alisema; “Taifa husomesha watu wake kwa faida ya Taifa.”

Amesema Serikali ya CCM kwa kutambua hilo, hadi kufikia Machi, 2024 imetoa Sh2.31 trilioni kutekeleza mpango wa  Elimumsingi bila ada ikiwa ni ruzuku tangu kuanza utekelezaji wa mpango huo Desemba, 2015. Kati ya fedha hizo Sh758.81 bilioni zimetolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Mchengerwa ametumia nukuu ya Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa kuzungumzia barabara za vijijini.

“…Naomba kunukuu maneno ya hayati Benjamin William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu kuhusu umuhimu wa barabara za vijijini alisema:

"Njia moja ya kuharakisha maendeleo ya vijiji ni kuhakikisha tunajenga na kuboresha barabara za vijijini. Barabara ni kiungo muhimu katika kuunganisha vijiji na huduma za kijamii kama shule, vituo vya afya na masoko.”

“Pia, barabara zinawezesha upatikanaji wa bidhaa za wakulima kwenye masoko na kuchochea biashara na ukuaji wa uchumi wa vijiji.”

“Hivyo, tusipuuze umuhimu wa barabara za vijijini katika juhudi zetu za kuendeleza maeneo ya vijijini."

Mchengerwa amesema  Serikali ya Awamu ya Sita kwa kulitambua hilo, imeendelea kuyaenzi maneno ya Rais Mkapa kwa kuendelea kutoa fedha kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) za ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara kutoka Sh275 bilioni mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh722.19 bilioni mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 163.44.

Kuhusu Nyerere

Mwalimu Nyerere alikuwa mtu mwenye kipawa na maadili. Alikuwa shujaa wa Afrika, mzalendo, aliyekuwa na kipaji cha kuzungumza, mwenye fikra imara, mwanadiplomasia na juu ya yote, alichangua kuitwa ‘Mwalimu’.

Akiwa madarakani, alitoa mamia ya hotuba; baadhi ziliandaliwa na nyingine bila kuandaliwa.

Taasisi ya Mwalimu Nyerere (aliyoianzisha Mwalimu Nyerere mwenyewe, mwaka 1996) imekusanya hotuba na maandiko yake kwenye vitabu.

Nukuu zilizomo katika kitabu, ni zile tu zilizomo katika mfululizo wa vitabu vya Uhuru na mihadhara yake ya chuo kikuu. Zimepangwa katika dhamira zifuatazo; falsafa, azimio, vijiji vya ushirika, kujitegemea, umoja na mshikamano, ujamaa, siasa za ndani, siasa za nje, demokrasia, elimu, uongozi, Serikali, Bunge, ulinzi na usalama, jamii na uchumi.