Mchengerwa: Kawachukulieni hatua wanaotumia mashine hewa za manunuzi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa. Picha na maktaba

Muktasari:

Imeelezwa kuna halmashauri zinatumia mashine hewa za manunuzi ama kuzizima wakati wa manunuzi na kuikosesha Serikali mapato.

Unguja.  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa amesema kuwa baadhi ya halmashauri zinatumia mashine hewa za kielektroniki kufanya manunuzi.

Mbali na halmashauri hizo zinazofanya ubadhirifu, zipo ambazo zimefanya vizuri katika makusanyo.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Aprili 23, 2024 alipokuwa  akifungua mkutano mkuu wa 38 Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika kwenye hoteli ya Golden Tulip mjini Unguja.

"Zipo mashine ambazo pengine nyinyi hamzijui kuwa ni hewa ila maofisa wenu wanazijua na zinazimwa wakati wa manunuzi na kuisababishia Serikali hasara.”

"Tunatambua kuwa zipo halmashauri zinatumia mashine feki kwa hivyo nendeni mukazidhibiti hizo kwa kuwachukulia hatua wenye tabia hiyo," amesema

 Amesema taratibu zote za manunuzi ya kikodi zinapaswa kuzingatia mifumo ya kielektroniki, ili kupunguza mianya ya rushwa na udanganyifu katika maeneo yao.

"Sitegemei kuwepo kwa halmashauri yeyote inayotumia  mifumo ya zamani, mategemeo yangu kwa kila mmoja wetu anafanya vizuri na kudhibiti hali hiyo," amesema  Mchengerwa.

Sambamba na hayo, Mchengerwa amesema miongoni mwao wapo wanaoweka makadirio ya kiwango cha chini, na kutokuwa na ubunifu wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato. 

Hivyo, amewataka viongozi hao baada ya kumaliza mkutano huo kwenda kufanya kazi mithili ya mchwa ili kutatua kero za wananchi na kusimamia miradi.

Pia, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, na kusisitiza kuchagua viongozi wazalendo, wenye weledi, wachapakazi na wasiokula rushwa.

Mchengerwa amewaagiza mameya, wenyeviti wa halmashauri kuondoa migogoro inapokuwepo kutumia ALAT kutafuta suluhu.

"Kumekuwepo na migongano kati ya wakurugenzi na madiwani, sisi sote tunajenga nyumba moja tunavutana nini huko?," amehoji Mchengerwa

Hata hivyo, amewaomba viongozi hao kutokuwa sehemu ya upotevu wa mapato, kwani yapo maeneo watu hawatoi risiti na kuhakikisha wanabaini wajanja wanaokwepa kodi.

Amesisitiza kwa viongozi hao kwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua ili uwe msingi wa utendaji wao.

Awali akisoma risala Makamu Mwenyekiti wa ALAT, Sima Constantine  Sima amesema jumuiya hiyo iliomba  kuongozewa posho na masilahi ya madiwani, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wa  Serikali za mitaa.

Amesema lengo la ombi hilo ni kuongeza tija ya ufanisi katika kuhamasisha na kusimamia shughuli za Serikali ili kufikisha matarajio kwa wananchi,

Pia ameomba kuongezewa fedha za matumizi mengine na kufanya semina elekezi ya kutambua wajibu wao.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa, Serikali za mitaa na idara maalumu za SMZ, Massoud Ali Mohammed amesema endapo Serikali za mitaa zikitengemaa vyema kwa kutambua majukumu yao,  bila kuwa na utashi wa kisiasa itaisaidia Serikali kuwafikia wananchi wake kwa urahisi.