Mchungaji kizimbani tuhuma za  udanganyifu

Mchungaji wa Kanisa la Joy's Testimony of Christ Church, lililopo Kigamboni, Godgiven Mushindikwa akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matano likiwemo la kuingia nchini kinyume cha sheria na kufanya kazi bila kuwa na kibali. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  •  Anakabiliwa na mashtaka matano yakiwamo ya kuwasilisha nyaraka za uongo ili kupata hati ya kusafiria.

Dar es Salaam. Mchungaji Godgiven Mushindikwa amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka matano, yakiwamo ya kufanya kazi ya uchungaji bila kibali na kuwasilisha nyaraka za uongo ili kupata hati ya kusafiria.

Mushindikwa (52), mchungaji wa Kanisa la Joy's Testimony of Christ lililopo Kigamboni, jijini hapa ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Amefikishwa mahakamani leo Aprili 17, 2024 na kusomewa kesi ya jinai namba 9767/2024, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.

Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphel Mpuya amedai Aprili 4, 2024 mshitakiwa aliingia nchini kinyume cha sheria.

Inadaiwa siku ya tukio, katika ofisi za Uhamiaji zilizopo Kurasini jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa ameingia nchini bila kibali au nyaraka yoyote inayoonyesha uhalali wa yeye kuwepo nchini.

Mpuya katika shtaka la pili, anadai akiwa eneo hilo, mshitakiwa alikutwa akiishi nchini bila ya kibali.

Amedaiwa katika shtaka la tatu, kuwasilisha nyaraka za uongo ofisi za Uhamiaji ili kujipatia hati ya kusafiria.

Wakili Mpuya amedai, siku na eneo hilo la tukio, mshitakiwa aliwasilisha ofisi ya Uhamiaji cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha Taifa (Nida), vyote vikiwa na jina la Godgiven, ambayo vilipatikana kwa njia ya uongo.

Imedaiwa katika shtaka la nne, mshitakiwa alidanganya kwa kuwasilisha nyaraka za uongo ili apate hati ya kusafiria.

Wakili mwingine wa upande wa mashtaka, Ezekiel Kibona katika shtaka la tano, alidai mshitakiwa alifanya kazi bila kuwa na kibali.

Amedaiwa Aprili 4, 2024, eneo la Kigamboni, akiwa raia wa DRC alikutwa akifanya kazi ya kiuchungaji katika Kanisa la Joy's Testimony of Christ bila kuwa na kibali.

Mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo na akaomba apewe dhamana.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi umekamilika, hivyo kuiomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya kumsomea maelezo ya ushahidi katika usikilizwaji wa awali.

Hakimu Mwankuga alitoa masharti ya dhamana ambapo mshitakiwa alitakiwa kuwa na  wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kila mmoja kutoka taasisi zinazotambulika kisheria, na kuwa na kitambulisho cha Nida.

Mshitakiwa amekamilisha masharti, hivyo  yupo nje kwa dhamana.

Hakimu Mwankuga ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 9, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.