Mengine yaibuka‘Flow meter’ bandari Dar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho.

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho amefanya ziara ya kushtukiza katika mtambo mpya wa kupimia mafuta (flow meter) uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam na kugundua hitilafu kadhaa, ikiwamo kuharibika kwa kamera zilizofungwa katika eneo hilo kwa zaidi ya mwezi.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho amefanya ziara ya kushtukiza katika mtambo mpya wa kupimia mafuta (flow meter) uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam na kugundua hitilafu kadhaa, ikiwamo kuharibika kwa kamera zilizofungwa katika eneo hilo kwa zaidi ya mwezi.

Ziara hiyo iliyohusisha baadhi ya watendaji wa Wizara iliibuka baada ya kuwapo tetesi za tukio lisilo la kawaida lililofanywa juzi na waangalizi wa mtambo huo mpya.

Hata hivyo, Meneja wa mradi, Mary Mhayaya alikiri kuwapo kwa tukio la kusafishwa chujio la mafuta lililopo ndani ya mtambo huo, kazi aliyosema ilifanywa na wafanyakazi wake kwa siku mbili na jana ilikuwa mwisho.

Mhayaya pia, alieleza kuwapo kwa tatizo la kuharibika kwa kamera mbili zilizoko kwenye mitambo hiyo na kwamba kuharibika huko hakuzuii mitambo hiyo kufanya kazi kwa kuwa kazi ya kamera hizo ni kumsaidia fundi kuona kinachoendelea maeneo ya nje.

Alisema mbali na kamera, waligundua tatizo la kuharibika valvu zilizoathiriwa na mvua na kusababisha mtambo huo kuendeshwa kwa nguvu ya nje badala ya kujiendesha.

Chamuriho alisema: “Nimetumwa na Waziri ili kuhakikisha vifaa vyetu vilivyowekwa na Serikali kwa ajili ya kulinda masilahi ya Serikali haviathiriki kwa lolote.”

Aliwataka waandae taarifa ya kila kinachoendelea katika mtambo huo sambamba na kueleza hitilafu zilizopo na waifikishe ofisini kwake Jumatatu asubuhi.

Chamuriho alisema mtambo huo ambao ulikuwa kwenye majaribio, umeanza kutumika na mpaka sasa tayari meli nne zimeshusha mzigo na unaonyesha umetoa vipimo sahihi.

Aliagiza kamera zote zilizoharibika zirudishwe na valvu hizo zibadilishwe kwa gharama za mkandarasi. “Hizo valvu ambazo zimeathiriwa na mvua azibadilishe maana kama alijua mtambo utakaa nje na lazima upigwe na mvua, alipaswa ahakikishe anaweka valvu ambazo hazitaathiriwa na mvua,” alisema.

Alisema upungufu mwingine waliougundua ni kutumia tangi la plastiki aina ya simtank kuhifadhi mafuta wakati wa kusafisha chujio, ambapo uwezo wa tangi hilo ni lita 5,000 jambo ambalo si kawaida wala si salama.

Chamuriho alisema sababu za kujengwa kwa mtambo huo ni kuhakiki ujazo wa mafuta unaotolewa ili kusaidia utozaji wa kodi na usawa wa mizigo ya wateja.