Mfumo wa kidigitali suluhisho kwa waomba ajira serikalini – Simbachawene

Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizumgumza na sekretarieti  Morogoro. Picha na Johnson James

Muktasari:

Inaelezwa kuwa ili kuondoa malalamika kuna haja sasa mfumo huo ukamuonyesha muombaji namna anavyokosa ajira

Morogoro. Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameiagiza sekretarieti ya ajira kuanza mchakato wa kuwa na mfumo mpya wa kurejesha matokeo ya usaili kidigitali.

Amesema hali hiyo itaondoa malalamiko kwa waombaji wa ajira mtandaoni katika mfumo ambao ulizinduliwa Februari, 2024.

Waziri Simbachawene amesema hayo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha Baraza la Sekretarieti ya Ajira mjini hapa.

Amesema ipo haja ya kuwajengea uelewa vijana wanaoomba ajira kupitia mfumo mpya wa ajira kujua kwamba, ajira hazitolewi kwa upendeleo.

"Natambua tulizindua mfumo wa ajira mtandaoni na sisi kama wizara tuliuzindua mfumo huo mkoani Manyara na kuufanyia majaribio nchi nzima, kwa kuwa umeshaanza kufanya kazi, nahitaji kuona mkiandaa mfumo mwingine wa kuonesha wale wanaokosa ajira wanakosa katika mazingira gani,” amesema.

“Hivyo, kuanzia sasa mlifanyie kazi tuone matokeo yake kwa kuwa hata Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa mifumo yetu isomane,” amesema.

“Malengo mahususi ya kuja na mfumo wa kuomba ajira mtandaoni ni kutaka ajira zitolewe kwa uwazi bila upendeleo, sasa kama tunatoa ajira kwa usahili ambao uko wazi lazima sekretarieti mje na mfumo utakaorejesha majibu kwa waliofanya usaili."

Awali, akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Ajira, Innocent Bomani wataendelea kuyafanyia kazi maelekezo yote wanayopatiwa na wizara.

"Tumepokea maelekezo ya kuja na mfumo mpya wa matokeo baada ya kufanya usaili mtandaoni, tutalifanyia kazi,” amesema.

Erasto Juma, mhitimu wa shahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na mkazi wa Kihonda mjini Morogoro, amesema: “Nimeshawahi kuomba ajira kupitia mfumo mpya wa kiserikali, nikakosa na sikupata mrejesho kwa nini sikuajiriwa, kama watakuja sasa na mfumo mwingine wa kutoa majibu kwa wale wanaokosa ajira itasaidia na itaondoa mawazo kuwa ajira zina wenyewe.”

Swaumu Simba, mhitimu wa shahada ya habari na mawasiliano kwa umma  amesema mfumo mpya wa kuomba ajira na kufanyiwa usaili mtandaoni ni mzuri lakini lazima Serikali ioneshe namna unavyofanya kazi.

“Binafsi naamini huu mfumo ni mzuri na hautakuwa na upendeleo lakini sisi wahitimu wengi wetu hatujui unavyofanya kazi, tuelimishwe,” amesema.