Mfungwa akutwa mtaani na nyara za serikali, bunduki

Muktasari:

  • Wakutwa na AK-47, Rifle, risasi 130 na meno ya tembo

Serengeti. Ni kawaida kukutana na wafungwa mitaani wakiwa wanasimamiwa na askari Magereza, lakini si kwa Kassim Musa Bheha; amekutwa mbugani akiwinda pamoja na wenzake watatu.

Bheha, ambaye ni mkazi wa Rufiji mkoani Pwani, alitakiwa kuwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu baada ya kutiwa hatiani katika shauri la uhujumu uchumi namba 5/2015. Lakini amekamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa), akituhumiwa kujihusisha na ujangili.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed aliwaambia waandishi wa habari mjini Mugumu jana kuwa mfungwa huyo na wenzake watatu walikamatwa saa 12:00 jioni ya Januari 3 katika Kijiji cha Robanda baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Aliwataja wengine wanaoshikiliwa kuwa ni wakazi wa vijiji vya Kono, Bwitengi na Robanda.

Kamanda Mohamed alisema watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na meno manne ya tembo yenye uzito wa kilo 72.4, bunduki mbili - moja ya kivita aina ya AK-47 na Rifle pamoja na risasi 130.

“Walikuwa na bunduki aina ya Riffle 458 na risasi tano zimefichwa katika uzio wa nyumba na baada ya mahojiano walikiri kuua tembo wawili ndani ya Hifadhi ya Serengeti Januari 2,” alisema.

Alisema baada ya kubanwa zaidi mmoja wa watuhumiwa hao aliwapeleka askari eneo walikokuwa wameficha bunduki aina ya AK-47.

Utata mfungwa kuwa nje

Akimzungumzia mfungwa huyo, Kamanda Mohamed alisema mtuhumiwa huyo ni mfungwa aliyepaswa kuwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu alichohukumiwa na Mahakama ya Hakimu MkaziWilaya ya Musoma mwaka jana.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wiki tatu baada ya kuhukumiwa, kuliibuka taarifa kuwa alipewa adhabu ya kifungo cha nje cha kutumikia jamii jijini Dar es Salaam ambako hata hivyo imebainika hajawahi kufika, suala ambalo pia polisi wamelianzishia uchunguzi.