Miili ya wanafamilia wanne waliokufa kwa mafuriko yaagwa Moshi

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye akiaga miili ya watu watano waliofariki kwa mafuriko Moshi katika viwanja vya KDC, vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.

Muktasari:

  •  Mwanafamilia asema wanamshukuru Mungu, angeweza kufuta kabisa kizazi cha familia lakini imempendeza kuacha baba, mama na mtoto mmoja

Moshi. Miili ya watu watano, minne ikiwa ya familia moja waliofariki dunia baada ya nyumba yao kuangukiwa na kifusi imeagwa mjini Moshi.

Kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia Aprili 25, 2024 nyumba yao iliangukiwa na kifusi.

Miili hiyo imeagwa leo Aprili 30, 2024 katika viwanja vya KDC, vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

April 25, kuliripotiwa vifo vya watu saba wakiwemo hao, baada ya mto Rau kujaa maji na kuvunja kingo, hivyo maji kusambaa kwenye makazi ya watu na mashamba.

Mvua ilisababisha nyumba kadhaa kuzingirwa na maji, hivyo kusababisha kaya 902 kukosa makazi, huku mifugo, vyakula na mali nyingine, zikisombwa na maji.

Kata za Mji Mpya, Msaranga, Kimochi, Kahe na Mabogini wilayani Moshi ndizo zilizoathiriwa.

Wanafamilia waliofariki duniani ni Anjela Chaki (12), Tito Chaki (63), Edward Chaki (14), na Fredy Justus (6).

Akizungumza kwa niaba ya familia, Jeremiah Chaki, ameishukuru Serikali kwa namna ilivyojitoa kwa hali na mali kuwasindikiza wapendwa wao katika safari yao ya mwisho duniani.

"Familia ya Chaki tunamshukuru Mungu kwa yaliyotukuta lakini ameendelea kutupa nguvu ya kuvuka, tunamshukuru kwa kuwa hata hili angeweza kufuta kabisa kizazi hiki cha Chaki, lakini imempendeza ameweza kuacha baba na mama na mtoto mmoja," amesema.

"Tunamshukuru mkuu wa wilaya kwa namna ambavyo ametukimbilia na kuhakikisha tunawapumzisha wenzetu salama, Mungu awabariki sana, tunaomba Watanzania ambao wameguswa na familia hii mtusaidie chochote kwa kuwa hakuna chochote ambacho familia imeweza kuokoa hata kijiji," amesema.

Akizungumza katika ibada ya kuaga miili hiyo, Mchungaji Javason Mrema wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) aliwatia moyo familia hiyo kutoka tamaa kwa kuwa bado Mungu anawapenda, akisisitiza wananchi kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji ili kuondokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Msikate tamaa kwa kuwa Mungu anawapenda, najua familia hii imepata pigo kubwa, kila mmoja asimame kwa nafasi yake kwa kuwa Mungu anatutunza, hivyo tumwombe aendelee kututia nguvu," amesema.

Kauli ya Mkuu wa Wilaya

Akizungumza wakati miili hiyo ikiagwa, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema Serikali itaendelea kutoa mkono wa pole kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao na kuwatahadharisha wananchi waliopo mabondeni kuondoka kabla madhara makubwa hayajajitokeza.

"Tumeendelea kuwa pamoja kuanzia siku ya kwanza ya tukio hili na tumeweza kuandaa kidogo ambacho kimeweza kufanya siku ya leo kuwaaga wapendwa wetu, tutaendelea kutoa mkono wa pole kwa familia ambazo zimefikwa na msiba huu mzito," amesema.

"Ndugu zangu akili za Mungu hazichunguziki sisi tumepewa akili lakini kuna wakati tunapiga kelele kuwataka watu waondoke mabondeni, watafute maeneo salama, ili kujiepusha na majanga ya asili yanapotokea tuwe salama zaidi," amesema.

"Nimetembea kwa miguu nilipokuwa nikienda Kijiji cha Lyakombila pale Kimochi nimejionea jinsi ambavyo mlima umeshiba maji lakini  miamba inatoa maji, kwa hiyo chemichemi nyingi zimeibuka na ukiona hivyo maana yake miamba hiyo inaendelea kuwa dhaifu, hivyo wananchi naomba mchukie tahadhari kwenye haya maeneo hasa kipindi hiki," amesema.

Amesema Serikali inaendelea kupambana kurudisha huduma za kawaida kwa wananchi waliokumbwa na madhara ya mvua ikiwemo utengenezaji wa miundombinu ya barabara na umeme, pia kurudisha huduma za maji kutokana na miundombinu yake kuathiriwa na mafuriko.

Sumaye amesema madhara bado ni makubwa, akieleza zaidi ya watu 4,400 wanahitaji vyakula, malazi nyumba na magodoro.

Amesema hali ni mbaya kwa kuwa hawakuweza kuokoa chochote kiilichokuwamo ndani.

"Serikali tunaangalia namna ya kuwasaidia kwa kuwapa chakula na magodoro ili kurejea katika hali zao za kawaida, uhitaji ni mkubwa sana,"

Pamoja na mambo mengine amewashukuru wadau waliojitokeza kuwasaidia waathirika hao wa mafuriko.

Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Enjoylight Mafuwe ameishukuru Serikali na jamii kwa namna ambavyo imewakimbilia katika kipindi kigumu wanachopitia.

"Tunaishukuru Serikali kwa misaada mbalimbali ambayo wametupa tangu tumepata mafuriko, lakini wadau ambao wamejitokeza kutusaidia, tunashukuru sana, maana tuliachwa watupu hakuna chochote tulichoweza kuokoa," amesema.

Elias Mshumbuzi, ambaye ni mwathirika wa mafuriko hayo, amewaomba wadau kuendelea kujitokeza kuwasaidia kwa kuwa hali zao bado ni ngumu na mahitaji bado mengi.