Morogoro kutunga sheria ndogondogo kudhibiti migogoro ya wakulima, wafugaji

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebecca Nsemwa.

Muktasari:

  • Serikali itaendelea kutatua changamoto kadiri ya uwezo wake katika maeneo yote na nyingine zinahitaji ushirikiano kama migogoro ya wakulima na wafugaji, uvamizi wa mali za vyama vya ushirika uliofanywa na wananchi.

Morogoro. Mkoa wa Morogoro upo katika hatua za kukamilisha utungaji wa sheria ndogondogo zenye lengo la kudhibiti wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao.

Pia imeelezwa kuwa  watakaobainika kuingiza mifugo kwenye mashamba  watakumbana na faini ya Sh100,000 kwa kila mfugo mmoja.

Akizungumza katika siku ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mkoani hapa leo Mei 9, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebecca Nsemwa amesema Serikali iko kwenye mchakato wa kukamilisha sheria na kanuni ndogondogo zenye lengo la kupunguza ama kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji.

Amesema kumekuwa na tabia za makusudi za baadhi wa wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba watakaobainika  watakutana na faini ya Sh100,000 kwa kila mfugo mmoja.

“Kila halmashauri itakabidhiwa sheria ambayo inalenga kupunguza ama kumaliza kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji ikiwemo ya mfugaji kuingiza mifugo makusudi kwenye shamba la mkulima.”

“Mifugo hiyo itahifadhiwa katika zizi ambalo litajengwa na Serikali na ndani ya siku saba endapo mfugaji atashindwa kulipa faini, itakuwa mali ya Serikali,” amesema.

DC Nsemwa ameongeza kuwa wakulima wamekata tamaa kwa baadhi ya maeneo wilayani  Mvomero, Kilosa na Kilombero kwa sababu ya mazao yao kuliwa na mifugo, hivyo sheria hizo zitaleta tija.

Mwanachama wa Chama cha Ushirika wa Kilimo cha Umwagiliaji Mpunga Dakawa (Uwawakuda), Asiao Namwela amesema kukamilika kwa sheria hiyo ndogo na kanuni zake itakuwa mkombozi kwa wakulima ambao wamekuwa wakiathirika kwa mashamba yao kuliwa na mifugo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Siku ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro 2024, Iddi Bilali amesema majukwaa ya ushirika kimkoa yaliasisiwa Februari, 2016 mjini Dodoma kwa lengo la kuwaleta wanaushirika pamoja ili kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili.

“Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Ushirika Hujenga Mustakabali Bora kwa Wote’ ikitoa msisitizo vyama vya ushirika kupata fursa ya kuonyesha michango yao katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ifikapo mwaka 2030,” amesema Bilal.

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Morogoro, Kenneth Shemdoe amesema mkoa huo una vyama vya ushirika 283, kati ya hivyo 215 ndiyo vimesajiliwa kwenye mfumo wa usimamizi wa vyama vya ushirika (Muvu) huku vyama 68 vikiwa havijasajiliwa.

Shemdoe amesema kutokana na ukubwa wa jiografia ya mkoa wa Morogoro ina upungufu wa maofisa ushirika 13 ili kuweza kukidhi ikama ya wataalamu 20 wanaotakiwa kuhudumu katika sekta ya ushirika mkoa.