Moshi Watahadharishwa mpasuko kuelekea chaguzi

Muktasari:

  • Madiwani na watendaji, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuwa wamoja na kuacha kutengenezeana ajali za kisiasa, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

Moshi. Madiwani na watendaji wa  Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuwa wamoja na kuacha kutengenezeana ajali za kisiasa, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi kitengo cha usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi wa fedha za miradi ya serikali, Ponceano Kilumbi wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.

Amesema ni hatari kubwa kwenda kwenye uchaguzi kukiwa na mgawanyiko na malumbano baina ya madiwani na madiwani na hata watendaji wa halmashauri.

Aidha amemtaka Meya wa Manispaa hiyo, Zuberi Kidumo kutengeneza utulivu kwa madiwani na kutumia rungu lake la mamlaka kuwashughulikia madiwani ambao wanaweka mpasuko na kuwatengenezea wenzao ajali, na kuhakikisha anatengeneza taasisi yenye afya.

"Ningeomba baraza la madiwani, watendaji na Mkurugenzi muwe kitu kimoja, hasa ninyi madiwani, ni lazima muwe kitu kimoja, tunakwenda kwenye uchaguzi na kama tunakwenda kwenye uchaguzi mwaka kesho halafu hatuko kitu kimoja siyo jambo lenye afya hata kidogo," amesema.

"Mstahiki meya, tengeneza utulivu, wakusanye hao viongozi ni wakwako, waweke pamoja, kwani tunakwenda kwenye uchaguzi, hatupaswi kutofautiana, hatupaswi kugawanyika wala hatupaswi kulumbana lumbana," amesema Kilumbi na kuongeza kuwa

"Kuna diwani mmoja amesema mnategesheana ajali, niwambie, mambo hayo yamepitwa na wakati, wewe Meya ni nafasi yako, ukiona kuna mtu ambaye anamtengenezea mwenzake ajali, tumia rungu yako ya mamlaka uliyopewa ili kutengeneza afya njema ya taasisi kwani tukienda kwenye uchaguzi na watu wa namna hiyo ni hatari," amesema.

Amesema, "Mambo kama hayo Meya wewe ndiye unapaswa kuyadhibiti, wewe ndiye umekabidhiwa rungu la kuweza kukomesha mambo yote ambayo ni maovu, tumia nafasi yako na kuhakikisha mnaungana na kuwa kitu kimoja.

Katika hatua nyingine, Kilumbi ameitaka Manispaa hiyo kuongeza nguvu katika kasi ya ukusanyaji wa mapato, na kueleza kuwa harakati zake za kuwa jiji hazitaweza kufanikiwa endapo wataendelea kuwa nyuma katika ukusanyaji wa mapato.

"Katika ripoti ya mwezi septemba, Manispaa ya Moshi imekuwa nyuma sana katika ukusanyaji wa mapato, ilikusanya kwa asilimia 20 na ilishika nafasi ya mwisho kimkoa katika ukusanyaji wa mapato, sasa tunapaswa kuongeza nguvu, tunapaswa kukimbia kwa sababu hatukufikia kiwango cha asilimia 25 ambacho kilihitajika katika robo ya kwanza," amesema.

Ameongeza kuwa, "Manispaa ya Moshi ni moja ya Manispaa ambazo zinapambana kuwa jiji, sasa Moshi tunaenda kuwa jiji kwa mapato ya Sh5 bilioni? amehoji na kueleza kuwa haitaweza kuwa jiji kwa mapato hayo hivyo wanapaswa kukimbia kuongeza ukusanyaji wa mapato," amesema.

Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine,  kulikuwa na mashauri ya kinidhamu kwa baadhi ya watumishi na madiwani,  agenda ambazo zilijadiliwa baada ya baraza kugeuka kuwa kamati.

Akisoma maazimio ya kamati ya Madiwani katika mashauri hayo ya kinidhamu, Meya wa Manispaa hiyo Zuberi Kidumo, amesema Madiwani waliokuwa wakituhumiwa walionywa na kutakiwa wasirudie makosa huku watumishi zikitakiwa kufuatwa taratibu za kisheria.

"Tulikuwa na agenda namba 7,8na 9, katika agenda hzo, yapo maazimio ambayo tumeyafikia, ambapo agenda namba 7 ilikuwa ni shauri la kinidhamu kwa baadhi ya watumishi, ambao wametajwa majina na kamati imeridhia taratibu za kisheria zifuatwe, lakini agenda ya nane ilikuwa ni shauri la kinidhamu dhidi ya madiwani wawili ambapo kwa mujibu wa kanuni na taratibu, kamati ya maadili ilitoa maoni yake na mapendekezo na tumeridhia maoni yaliyotolewa na kamati hiyo ya maadili,"amesema Kidumo.

"Lakini agenda namba tisa ilikuwa ni shauri la kinidhamu la diwani mmoja ambapo pia kwa kujibu wa taratibu kamati ya maadili ilitoa maoni na mapendekezo yake na kwa pamoja kamati ya madiwani iliridhia na kupendekeza ushauri uliotolewa na kamati ya maadili uzingatiwe na kufuatwa. Pia litolewe onyo na kuzungumza nao ili wasirudie yale yaliyobainika katika tuhuma zao," amesema.