Moto wa kikokotoo washika kasi kutaka mabadiliko

Tanga/Moshi. Jinamizi la kikokotoo linazidi kuwatafuna wafanyakazi tangu kanuni mpya za mwaka 2018 zianze kutumika, jambo lililowagusa pia watumishi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini wanaotaka yafanyike maboresho kwa kuwa kinawaathiri wanapostaafu.

Kundi hili limeibuka siku chache baada ya askari Polisi nchini nao kupaza sauti wakitaka waondolewe katika malipo ya mkupuo ya asilimia 33, walipwe fedha zao zote kwa mkupuo kama Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Katika kudhihirisha kikokotoo ni kaa la moto na kinaibua hisia na hali tete kwa wafanyakazi, Desemba 2018, Rais wa awamu ya tano, John Magufuli aliliona hilo na kuamua kusitisha matumizi ya kikokotoo hicho.

Hata hivyo, Mei 26, 2022, Katibu Mkuu ofisi ya Waziri mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Jamal Katundu alitangaza kuanza kwa kikokotoo kipya, akisisitiza kikokotoo cha mafao ya mkupuo kwa mifuko yote kitakuwa ni asilimia 33.

Tangu wakati huo, kumekuwepo na kilio kisichokoma cha wafanyakazi na takribani siku 10 zilizopita, askari Polisi kutoka maeneo mbalimbali nchini waliliibua upya wakidai suala hilo linaathiri morali ya kufanya kazi.

Polisi hao, hususan wa vyeo vya kuanzia Inspekta hadi Koplo, walitaka sheria inayotumika kuwalipa mafao askari wa JWTZ na JKT wanaolipwa mafao yao yote kwa mkupuo kwa asilimia 100, ndiyo ingetumika kwao ili kuleta usawa wa majeshi.

Lakini Septemba 4, 2023 akiwa Oysterbay jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua kikao kazi cha maofisa waandamizi wa Polisi, Rais Samia alipokea kilio cha kikokotoo kutoka kwa askari hao, kupitia nyimbo zilizoimbwa na askari hao walipokuwa wanaburudisha wageni kwenye hafla hiyo.

“Mama kikokotoo kiangalie hakika kitatuua. Maana wastaafu wengi huko nje wanalia. Hakika uamuzi wako ni wa busara, tunangoja huruma yako uweze kutusaidia,” ilisema sehemu ya mashairi ya moja ya nyimbo zilizoimbwa na askari hao kwenye hafla hiyo.

Wiki iliyopita, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na kumuuliza nini kinaendelea baada ya kauli ya Rais? Akajibu kuwa kwa kuwa Rais ameshatoa maelekezo, wahusika wasubiri utekelezaji.


Vyuo Vikuu nao waliamsha

Katika kuonyesha sakata la kikokotoo ni moto, leo Desemba 19, 2023 jijini Tanga watumishi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu waliomba kanuni ya kikokotoo ifanyiwe marekebisho, kwani inawaathiri kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwa na mishahara midogo.

Mbali ya kikokotoo hicho, lakini watumishi hao wameiomba Serikali kuweka uwiano sawa katika kuhudumia vyuo vikuu binafsi, badala ya kuegemea zaidi vyuo vikuu vya Serikali kwa kuwa vyote vinawahudumia vijana wa Tanzania.

Watumishi hao walitoa maombi hayo walipozungumza na Mwananchi ambapo wamekutana kuhudhuria mkutano wa 15 wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) uliofanyika jijini Tanga.

Mwenyekiti wa THTU, Dk Paul Loisulie alisema wanajipanga kufanya mazungumzo na Serikali ili kuomba ufanyike mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria ya kikokotoo.

"Marekebisho yafanyike, tunaathirika kutokana na mishahara yetu tunatoka mikono mitupu," amesema Loisulie.

Kwa mujibu wa Dk Loisulie, changamoto nyingine wanayokumbana nayo watumishi wa vyuo vikuu na taasisi zake ni mkanganyiko uliopo wa kuwa chini ya vyombo viwili tofauti ambavyo ni Msajili wa Hazina na Utumishi.

"Tunapendekeza tubaki chini ya Msajili wa Hazina ili tuondoke njiapanda. Tukibaki kama zamani hata muundo wa mishahara unaweza kurekebishwa na kujikuta tukifurahia utumishi wetu,” ameeleza.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa kamati ya THTU, Salma Fundi alisema jumla ya wajumbe 100 kutoka vyuo vikuu na 49 kutoka taasisi za elimu ya juu wamekutana jijini Tanga kuhudhuria mkutano huo ulioambatana na mkutano Mkuu wa 14.