Mpwapwa waahidiwa gari la wagonjwa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Serikali imeahidi kupeleka gari la wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Mpwapwa katika mwaka wa fedha 2022/23.

Dodoma. Serikali ya Tanzania, imeahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma katika mwaka wa fedha 2022/23.

 Ahadi hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne, Septemba 13, 2022 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Festo Dugange.

Naibu Waziri ametoa majibu hayo kufuatia swali la mbunge wa Mpwapwa George Malima ambaye amehoji ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa katika hospitali hiyo ambayo licha ya kuhudumia wilaya kubwa lakini haina gari.

Malima ameeleza uchakavu wa majengo katika hospitali hiyo akiomba Serikali itamke ni lini itapeleka fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa majengo.

Naibu Waziri amekiri hospitali hiyo inastahili kuwa na gari la wagonjwa na kwamba kipaumbele kitawekwa kwenye wilaya hiyo ili mapema iwezekanavyo ipelekwe gari huko.

"Kuhusu majengo na kwenda kujionea majengo hayo, naomba niahidi niko tayari kutembelea hospitali hiyo ili kujionea mahitaji ya ukarabati wa majengo ingawa mwezi wa nne nilitembelea wilaya hiyo," amesema Dk Dugange.

Kuhusu ukarabati wa majengo ya hospitali zingine, amesema Serikali imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati huo maeneo mengi.